Wenyeji wa Kombe la Dunia wakosa tikti ya kusonga mbele
23 Juni 2010Licha ya Afrika Kusini kuifunga Ufaransa mabao 2-1 katika mchezo wa hiyo jana, mjini Johannesburg, wenyeji hao wametimuliwa kwa sababu ya tofauti ya pointi za jumla.
Hata hivyo "Bafana Bafana" waliweza kuondoka uwanjani kwa fahari kinyume kabisa na Ufaransa iliyofunga virago na kurejea nyumbani kwa fedheha.
Nigeria pia haikufanikiwa kusonga mbele licha ya kwenda sare ya mabao 2-2 ilipopambana na Korea ya Kusini hiyo jana mjini Durban. Timu nyingine iliyotimuliwa hiyo jana ni Ugiriki iliyochuana na Argentine na kufungwa mabao 2-0.
Lakini ngoma ipo leo hii pale Ujerumani na Ghana zitakapoteremka uwanjani kucheza kufa kupona ili kuweza kujipatia tikti ya kuingia katika duru ya pili ya michuano hiyo ya Kombe la Dunia.
Uingereza nayo inafahamu kuwa leo haina budi kushinda itakapokumbana na Slovenia au itajiona ikifunga virago na kurejea nyumbani katika duru ya mwanzo ya michuana ya kuwania Kombe la Dunia.
Michezo mingine ya leo hii ni Marekani dhidi ya Algeria na Australia nayo itapambana na Serbia.