1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri Westerwelle ziarani Mashariki ya Kati

8 Novemba 2010

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle aliewasili Israel siku ya Jumapili, amekutana na waziri mwenzake wa Israel Avigdor Liebermann mjini Jerusalem.

https://p.dw.com/p/Q1Lj
Israeli Foreign Minister Avigdor Lieberman, right, and his German counterpart Guido Westerwelle attend a joint press conference in Jerusalem, Sunday, Nov. 7, 2010. (AP Photo/Sebastian Scheiner)
Waziri wa Nje wa Ujerumani Guido Westerwelle na waziri mwenzake wa Israel Avigdor Liebermann kwenye mkutano wa pamoja na waandishi wa habari mjini Jerusalem.Picha: AP

Vile vile alikutana na Rais wa Israel, Shimon Peres na familia ya mwanajeshi wa Kiisraeli Gilad Shalit anaezuiliwa mateka katika Ukanda wa Gaza tangu mwaka 2006. Westerwelle ametoa mwito kwa Israel kupunguza vikwazo vilivyowekwa dhidi ya Ukanda wa Gaza na kuruhusu bidhaa za Wapalestina kusafirishwa nje. Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani,Guido Westerwelle ametoa mwito kwa Waisraeli na Wapalestina kuimarisha jitahada za kuendeleza majadiliano ya ana kwa ana kati ya pande hizo mbili. Mchakato wa amani wa Mashariki ya Kati hauwezi kuruhusiwa kukwama. Westerwelle alitamka hayo kwenye mkutano wa waandishi wa habari uliofanywa pamoja na waziri mwenzake wa Israel Liebermann mjini Jerusalem. Vile vile alikiri kuwa bado anatofautiana na mwenyeji wake katika suala la makaazi ya walowezi wa Kiyahudi.Amesema:

"Serikali ya Ujerumani inaendelea kufuatilia suluhisho la mataifa mawili kamili yenye haki, kwa hivyo hata kati ya marafiki inaruhusiwa kuongezea kuwa katika tatizo la makaazi tumekuwa na misimamo tofauti."

Liebermann akathibitisha kwa matamashi haya:

"Kwa ufupi ningesema kuwa hatukuafikiana katika suala la makaazi, lakini kwangu mie ni wazi kuwa makaazi si kikwazo kwa amani."

Westerwelle alieuleza uhusiano wa pande hizo mbili kuwa ni mzuri sana, alitoa mwito kwa Israel kuondosha vikwazo vilivyowekwa dhidi ya Ukanda wa Gaza miaka mitatu na nusu iliyopita na kuruhusu bidhaa za Wapalestina kusafirishwa nje. Amesema, Wapalestina wanahitaji kuwa na matumaini ya kupatikana hali bora ya kiuchumi ili mchakato wa amani uweze kufanikiwa. Wapalestina wenye misimamo ya wastani waimarishwe - na hapo kunahitajiwa maendeleo ya kiuchumi yaliyo bora zaidi. Kwa hivyo, ametoa mwito wa kuruhusu bidhaa za Ukanda wa Gaza kusafirishwa nje.

Leo Westerwelle ametembelea shule ya wasichana na mtambo wa kusafishia maji machafu unaojengwa Gaza kwa msaada wa Ujerumani. Vile vile amekutana na wafanyabiashara kujadili matatizo ya kiuchumi yanayokabiliwa katika eneo hilo. Westerwelle ni waziri wa kwanza wa Ujerumani kwenda Ukanda wa Gaza tangu mwaka 2006.

Mwandishi: Verenkotte,Clemens/ZPR

Mpitiaji: Josephat Charo