1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri wa ulinzi wa Marekani awasili nchini Afghanistan

Kabogo, Grace Patricia11 Desemba 2008

Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Robert Gates amewasili nchini Afghanistan, ambako Marekani inaangalia uwezekano wa kuongeza jeshi lake ili kukabiliana na ongezeko la mapigano.

https://p.dw.com/p/GDb5
Baadhi ya wanajeshi wa Marekani walioko nchini AfghanistanPicha: AP

Bwana Gates amesema Marekani ina mpango wa kupeleka wanajeshi zaidi wapatao 7,000 nchini Afghanistan katika majira ya joto hapo mwakani, lakini lazima ifanye jitihada zaidi kuishirikisha Afghanistan katika kudhibiti ongezeko la mapigano.


Waziri huyo wa Marekani anaetembelea ngome ya jeshi la nchi za jumuiya ya NATO kusini mwa Afghanistan katika mji wa Kandahar, amesema alikuwa anafanya kazi ya kushughulikia ombi la kuongezwa majeshi zaidi, lililotolewa na Jenerali David Mckiernan, kamanda wa juu wa Marekani katika majeshi hayo nchini Afghanistan.


Wanajeshi hao watakuwa ni nyongeza ya vikosi viwili vya brigedi vinavyotarajiwa kupelekwa nchini Afghanistan mwezi Januari, mwaka ujao wa 2009.


Hata hivyo, Waziri Gates amesema utawala ujao wa Rais mteule wa Marekani, Barack Obama unapaswa kuwa makini katika upelekaji wa majeshi zaidi ya kimataifa nchini Afghanistan, ambayo mara nyingi hatua kama hiyo inashindikana. Gates, ambaye ataendelea kushika wadhifa wake huo katika utawala ujao wa Obama, amesema amekuwa akiwasiliana na Bwana Obama, lakini mazungumzo yao binafsi na bado hawajazungumzia suala lolote kuhusu sera za kigeni au masuala ya usalama wa nchi hiyo.


Ameongeza kuwa historia ya majeshi ya kimataifa nchini Afghanistan, ambayo imekuwa ikionekana kama ni kwa malengo yao binafsi, siyo nzuri. Uvamizi nchini Afghanistan uliongozwa na Marekani kufuatia mashambulio ya nchini humo ya Septemba 11, mwaka 2001, yalimuondoa madarakani kiongozi wa kundi la Taliban nchini Afghanistan, mwishoni mwa mwaka 2001. Lakini tangu wakati huo wapiganaji wamekuwa wakiendeleza vita dhidi ya wanajeshi hao wanaoiunga mkono serikali ya Rais Hamid Karzai wa nchi hiyo.


Kwa sasa kuna wanajeshi wa kimataifa wapatao 65,000 nchini Afghanistan, ambapo 31,000 ni kutoka Marekani, wakifanya kazi ya kuweka hali ya usalama nchini humo kutokana na kuongezeka kwa mapigano yanayofanywa na kundi la Taliban na wapiganaji wengine.


Uwezekano wa Marekani kupeleka majeshi zaidi nchini Afghanistan, bado unategemea kwa kiasi kikubwa kuondolewa kwa majeshi ya nchi hiyo Iraq.


Obama anayepinga vita nchini Iraq amesema anataka majeshi ya Marekani kuondoka nchini Iraq ndani ya kipindi cha miezi 16, lakini suala hilo litategemeana na ushauri atakaopewa na maafisa wa kijeshi.


Aidha, Gates amedokeza kwamba mkakati wa Afghanistan ulioangaliwa upya na utawala wa Rais George W. Bush, utatumiwa vile vile na utawala wa Obama, utakaochukua rasmi madaraka Januari 20, mwaka ujao.