Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Condoleeza Rice amaliza ziara ya Mashariki ya Kati | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 27.03.2007
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Timu Yetu

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Condoleeza Rice amaliza ziara ya Mashariki ya Kati

Baada ya siku nne za harakati za kidiplomasia katika mashariki ya kati, waziri wa mambo ya nje wa Marekani Condoleeza Rice ametoa mwito kwa nchi za kiarabu kuisogelea Israel ili kuendeleza mchakato wa amani katika eneo hilo.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Condoleeza Rice

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Condoleeza Rice

Baada ya siku hizo nne waziri Rice pia ametaarifu kuwa waziri Mkuu wa Israel Ehud Olmert na rais wa mamlaka ya Palestina bwana Mahmoud Abbas wamekubaliana kukutana kila baada ya wiki mbili.Bibi Rice amesema kuwa yeye pia atashiriki kwenye mikutano hiyo mara kwa mara.

Ameeleza kuwa Marekani inaweza kushirikiana na serikali ya Umoja ya Palestina , lakini kwa mara nyingine amesisitiza msimamo wa nchi yake juu ya kukitaka chama cha Hamas kiache siasa ya kutumia nguvu. Chama hicho bado kinakataa kuitambua Israel aidha hakitambui bayana makubalino yaliyofikiwa na Isreal mnamo miaka ya nyuma .

Akizungumza na waandishi habari mjini Jerusalem katika kituo cha mwisho cha ziara yake waziri Condoleeza Rice amesisitiza ulazima wa nafasi ya Israel kutambuliwa katika mashariki ya kati.

Amesema nchi za kiarabu hazina budi zianze kuisogelea Israel ili kuipa nchi hiyo uhakika kwamba itakuwa na usalama zaidi hata baada ya kuundwa nchi ya wapalestina. Nchi za kiarabu zinapaswa kutambua nafasi ya Israel na kuonesha kwamba amani maana yake ni zaidi ya kutokuwapo vita.

Amesema hatua ya ujasiri ya kuisogelea Israel itazibadili kauli za Umoja wa nchi za kiarabu kuwa msingi wa diplomasia ya nguvu itakayoharakisha hatua za kufikia siku ya kuundwa nchi ya wapalestina, itakayoshiriki kwa haki zote katika jumuiya ya kimataifa.

Pamoja na kufanikiwa katika makubaliano ya mikutano ya kila baada wiki mbili baina ya waziri mkuu wa Israel Ehud Olmert na rais wa mamlaka ya Palestina bwana Mahmoud Abbas, waziri Condoleeza Rice amekiri kuwa juhudi za kuanzisha tena mazungumzo ya amani zinatatanishwa kutokana na serikali mypa ya Palestina ambapo chama cha Hamas pia kinashiriki.

Chama hicho kinatathminiwa kuwa kundi la kigaidi na nchi za magharibi na hasa na Marekani.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani bibi Condoleeza Rice alianza ziara yake mapema jumamosi kwa kukutana na viongozi wa Misri,Saudi Arabia,Jordan na Falme za kiarabu kwa lengo la kufufua mpango wa amani wa nchi za kiarabu kwenye mkutano wa viongozi wa Umoja wa nchi hizo unaotarajiwa kufanyika kesho mjini Riyad.

Na Abdu Mtullya

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com