1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri Mkuu wa Ethiopia ajigamba juu ya nguvu za kijeshi

6 Julai 2021

Waziri Mkuu wa Ethiopia amejigamba kuwa serikali yake ina uwezo wa kuajiri kwa urahisi wapiganaji wapya milioni moja lakini kwanza anataka kuwepo kwa kipindi cha ukimya katika jimbo lililokumbwa na vita la Tigray.

https://p.dw.com/p/3w4mh
Äthiopien Premierminister Abiy Ahmed
Picha: Mulugeta Ayene/AP Photo/picture alliance

 Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed amejigamba kuwa serikali yake ina uwezo wa kuajiri kwa urahisi wapiganaji wapya milioni moja lakini kwanza anataka kuwepo kwa kipindi cha ukimya katika jimbo lililokumbwa na vita la Tigray. Abiy pia ametilia mkazo kuimarishwa kwa jeshi la nchi hiyo na kutoa wito kwa vijana kujiunga na jeshi.

Soma zaidi:Waasi wa Tigray wakubali kusitisha mapigano kwa masharti

Kauli ya mshindi huyo wa tuzo ya amani ya Nobel ya mwaka 2019 ameitoa wiki moja tu baada ya mji mkuu wa jimbo la Tigray wa Mekele kuwa chini ya udhibiti wa viongozi wa waasi na pia serikali kutangaza kusitisha mapigano yaliyodumu miezi nane.

Abiy amesema "Iwapo wapiganaji wanahitajika, katika muda wa mwezi moja au miwili, basi kikosi maalum cha wapiganaji kinaweza kuajiriwa. Vijana milioni moja wanaweza kukusanywa na kupokea mafunzo ya kijeshi."

Hata hivyo, Waziri Mkuu huyo amesema wameamua kuwepo kwa kipindi cha ukimya ili kila mtu afikirie.

"Tunapoangalia jinsi hali ilivyo sasa Tigray, naona kuna wengi wasiotaka mzozo huo kuisha. Kuna wale ambao wanataka tuishi katika mizozo na kuiona Ethiopia ikiharibika na Tigray iliyoharibiwa. Pia, kuna wengine wanaotaka kuona Oromia na Amhara zilizoharibiwa. Huo ndio mtazamo wetu. Kwa kweli, kuna watu wanatutakia mabaya."

Abiy ametoa wito kwa vijana kujiunga na jeshi

Äthiopien Tigray Soldaten Kämpfer
Wapiganaji wa Amhara wanaounga mkono jeshi la EthiopiaPicha: Eduardo Soteras/AFP/Getty Images

Katika hotuba yake bungeni wakati wa kura ya kuidhinisha bajeti ya serikali, Abiy aliliminia sifa jeshi la Ethiopia kwa kuonyesha uzalendo.

Viongozi wa waasi wa Tigray walielezea kuchukua tena udhibiti wa Mekele na sehemu kubwa ya mkoa wa kaskazini wa Tigray kama ushindi mkubwa, japo Waziri Mkuu Abiy pamoja na maafisa wengine wamedai kuwa, kuondoka kwa vikosi vya jeshi katika jimbo hilo ulikuwa mpango wa kimkakati wa kushughulikia vitisho vya usalama katika sehemu nyengine.

Mnamo siku ya Jumapili, viongozi hao waasi walitoa rasmi jibu lao juu ya wito wa kusitisha mapigano, wakisema wako tayari kuweka chini silaha japo kwa masharti ikiwa ni pamoja na kuondoka kwa vikosi vya Eritrea na wapiganaji kutoka jimbo jirani la Amhara, ambao wamekuwa wakiliunga mkono jeshi la Ethiopia.

Pia walimtaka Abiy na Rais wa Eritrea Isaias Afwerki kuwajibishwa kwa uharibifu uliosababishwa wakati wa mzozo huo ulioshuhudia umwagaji damu na visa vya unyanyasaji wa kijinsia.

Abiy hata hivyo alifumbia macho masharti hayo katika hotuba yake bungeni.

Maelfu ya watu wameuawa na wengine wengi wanakabiliwa na baa la njaa tangu mzozo huo ulipoanza Tigray, sehemu inayotajwa kuwa muhimu kiuchumi na kiviwanda katika taifa hilo la Pembe ya Afrika.