1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wavenezuela wapinga pendekezo la Rais wao Hugo Chaves la kutaka mabadiliko ya katiba ya nchi hiyo.

Halima Nyanza3 Desemba 2007

Rais Hugo Chavez wa Venezuela ameshindwa kufuatia matokeo ya kura zilizopigwa, kuhusu mabadiliko ya katiba ya nchi hiyo yaliyopendekezwa na Rais huyo, na kwamba ameelezea kuyakubali matokeo hayo yaliyopinga wazo lake.

https://p.dw.com/p/CWIi
Rais Hugo Chaves akiwapungia wafuasi wake, ambao kura zao hazikutosheleza kufanikisha mapendekezo yake ya kubadili katiba ya nchi hiyo.Picha: AP

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari mara baada ya matokeo hayo kutangazwa Rais Chavez aliwataka wafuasi wake kutojisikia vibaya baada ya kushindwa, kutokana na kwamba walikuwa wameshindwa kwa kura chache tu.

Kwa mujibu wa Tume ya taifa ya uchaguzi nchini humo tofauti ya kura ilikuwa ni asilimia 51 kwa 49 na kwamba asilimia 44 ya watu waliojiandikisha kupiga kura hawakujitokeza katika zoezi hilo.

Rais Chavez ameeleza wazi kwamba pendekezo hilo alilolitoa la kubadilisha katiba ya nchi hiyo kwa upande wake bado liko pale pale licha ya kushindwa katika zoezi hilo la upigaji kura.

''Kwa leo hatujafanikiwa, lakini tunaendeleza mapambano kwa ujenzi wa ujamaa. Pendekezo la Katiba mpya bado linabaki kuwa pendekezo langu na la umma wa Venezuela. pendekezo hili bado ni hai na halijafa''

Hii ni mara ya kwanza kwa Rais Chavez kuanguka katika kura tangu aingie madarakani mwaka 1999, baada ya watu waliokuwa hawaungi mkono mabadiliko ya katiba aliyokuwa akiyataka kushinda katika zoezi hilo la kupiga kura.

Miongoni mwa mabadiliko yaliyopendekezwa na Rais Hugo Chavez ni pamoja na kutokuwepo kwa ukomo wa kugombea urais na kusitisha uhuru wa Benki Kuu ya nchi hiyo.

Wapinzani waliokuwa wakipinga mabadiliko hayo wameonekana wakishangilia ushindi huo kwa kurusha fataki hewani na nderemo nyingine kadhaa mara tu baada ya matokeo kutangazwa katika mitaa ya mji wa Caracas.

Matokeo hayo yanadhihirisha jinsi pendekezo hilo la Rais Chevez la katiba mpya lilivyoleta mvutano mkali miongoni mwa Wavenezuela.

Awali kabla ya matokeo Rais Chavez alieleza kuwa atakubaliana na matokeo yoyote yatakayotangazwa.

Akiyatetea mababdiliko hayo Rais Chavez alisema yataupa umma madaraka zaidi, lakini wapinzani wake walipinga kauli hiyo..

Chavez ambaye ni mkosoaji wa sera za Marekani, akishirikiana na Cuba na Iran, anadaiwa kutaka mabadiliko hayo ya katiba ya nchi hiyo yenye utajiri mkubwa wa mafuta ili kuweza kuendelea kuongoza hata baada ya muda wake kumalizika, baada ya awamu mbili za kukaa madarakani.

Imedaiwa kuwa, Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 53 alitaka kubadilisha katiba ya nchi hiyo ili kuweza kutawala nchi hiyo mpaka mwaka 2050 atakapokuwa na miaka 95.

Mabadiliko mengine yaliyopendekezwa na Rais Chavez ni kuwa na sauti zaidi katika jeshi la nchi hiyo.

Wapinzani wake wamekuwa wakimlaumu kwamba amekuwa akitaka kubadilisha mkatiba ya nchi hiyo ili kuweza kuweka taifa hilo katika utawala wa kidikteta.