1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu zaidi ya 12 wauwawa California

Saumu Mwasimba
8 Novemba 2018

Mtu aliyekuwa na bunduki ndie aliyehusika kuua watu hao 12 akiwemo afisa wa polisi baada ya kuwashambulia kwa kuwapiga risasi watu kwenye bar ya muziki

https://p.dw.com/p/37uLW
USA, Kalifornien: Schießerei in Thousand Oaks
Picha: Reuters/R. Chiu

Nchini Marekani mtu aliyekuwa na bunduki amewauwa watu 12 akiwemo afisa mmoja wa polisi baada ya kuwashambulia kwa kuwapiga risasi watu kwenye bar ya muziki wa asili wa Kimarekani iliyokuwa imefurika wanafunzi wa chuo huko California. 

Tukio hilo limetokea katika eneo linaloitwa Thousand Oaks huko California jumatano usiku kwa saa za Marekani ambapo imeripotiwa mshukiwa alirusha mabomu ya kutoa moshi ndani ya bar hiyo ambayo usiku huo ilikuwa imefurika wanafunzi waliokuwa wakifurahia muziki wa Country. Polisi imetoa maelezo zaidi  kuhusu kilichotokea.

 

''Wakati polisi wa ziada walipowasili kwenye eneo la tukio walifanikiwa kuingia ndani wakakuta wahanga 11 waliokuwa wameshauwawa mtu anayeaminika kuwa ndiye mshukiwa pekee alikuwa amekufa hukohuko ndani.Na watu wengine kadhaa walikutwa na majeraha ya aina mbali mbali walichukuliwa na kupelekwa kwenye hospitali za eneo hilo''

Kalifornien Thousand Oaks Schießerei Nachtclub
Picha: picture-alliance/AP Photo/KABC

Mshukiwa aliyefanya shambulizi hiyo bado hajatambuliwa ni nani haswa na kwa mujibu wa afisa mkuu wa polisi katika eneo hilo dhamira ya mshambuliaji huyo pia haijajulikana. Tukio hili la mauaji ya  watu wengi kwa kupigwa risasi  ni la pili  nchini Marekani katika kipindi cha chini ya wiki mbili. Mashahidi wanasema kwamba mtu aliyekuwa na bunduki akiwa amevaa gwanda jeusi lililomfunika juu mpaka chini alirusha bomu la moshi ndani ya bar ya Borderline kabla ya kuanza kufyetua risasi saa tano na dakika 20 usiku Jumatano.

Mkuu wa kituo cha polisi cha kaunti ya Ventura Geoff Dean pia amewaambia waandishi habari kwamba hawafahamu ikiwa kuna uhusiano wowote wa tukio hilo na ugaidi mpaka kufikia wakati huu na kwamba uchunguzi unaendelea. Ingawa pia ameweka wazi kwamba hakuna kitu kinachomfanya yeye au maafisa wa shirika la upelelezi wa ndani FBI kuamini kwamba linahusiana na ugaidi.

Polisi ambaye ni miongoni mwa watu waliouwawa, Ron Helus, ametumikia kikosi chake kwa miaka 29 na ndie aliyekuwa afisa wa kwanza wa usalama kufika kwenye eneo la tukio. Ni siku 10 tu zimepita tangu mshambuliaji mwingine kuvamia na kuwauwa kwa kuwapiga risasi waumini 11 katika sinagogi la wayahudi huko Pittburg. Mshambuliaji Robert Bower aliyesema alikuwa akitaka kuwawa wayahudi alidai kwamba kundi la wanaharakati wa kiyahudi walikuwa wakiwasaidia wahamiaji. Rais Trump ameandika ujumbe wa Twitta akitoa salamu za pole kwa waliofikwa na msiba na waliojeruhiwa huko Carlifornia

Mwandishi: Saumu Mwasimba

Mhariri: Mohammed Khelef