1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu watatu wafariki Uganda katika ghasia za uchaguzi

Lubega Emmanuel 19 Novemba 2020

Polisi nchini Uganda imethibitisha vifo vya watu watatu kutokana na machafuko yaliyozuka alasiri ya Jumatano kufuatia habari za kukamatwa kwa mgombea urais Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine

https://p.dw.com/p/3lXXS
Uganda Festnahme Robert Kyagulanyi aka Bobi Wine
Picha: Abubaker Lubowa/REUTERS

Machafuko hayo yalisambaa katika miji kadhaa na kusababisha watu wengi kujeruhiwa kutokana na risasi na mabomu ya kutoa machozi. Hii imewalazimu wagombea wawili kwa kiti cha urais kusitisha kampeni zao hadi pale mwenzao atakapoachiwa.

Mayowe yalifuata machafuko yaliyozuka hapo siku ya Jumatano katika miji ya Kampala, Jinja, Tororo, Mbale, Soroti na Masaka. Hii ni baada ya watu kadhaa kubainika kupoteza maisha yao huku wengine wakipata majeraha mabaya sana.

Ijapokuwa habari mbalimbali kwenye mitandao ya kijamii na zile kutoka shirika la msalaba mwekundu zinaelezea kuwa angalau watu 11 waliuawa, jeshi la polisi limetoa taarifa kuwa ni watu watatu tu waliopoteza maisha yao na bado wanachunguza chanzo cha vifo vyao. Polisi inawalaumu wagombea urais na wafuasi wao kwa kuwachokoza na kusababisha hata askari wenzao kujeruhiwa katika machafuko hayo hayo ni kulingana na Msemaji wa polisi Fred Enanga.

Uganda Festnahme Robert Kyagulanyi aka Bobi Wine
Mgombea urais wa Uganda Bobi Wine alipokamatwa na polisiPicha: Abubaker Lubowa/REUTERS

Hata hivyo wanaharakati wa haki za binadamu wanasisitiza kuwa polisi na majeshi walitumia nguvu za kupindukia katika kukabiliana na makundi ya wafuasi katika miji mbalimbali na kusababisha wengi kujeruhiwa. Wanaelezea kuwa mazingira ya kampeni ni ya shamrashamra na watu hawawezi kudhibitiwa hisia zao za kushangilia wagombea na ukiwatatiza basi hisia hizo zinageuka kuwa za ghadhabu.

Katika mojawapo ya visa, gari lililokuwa na rangi za chama tawala cha NRM liliwagonga na kuwasababishia majeraha mabaya watu katika eneo lenye shughuli nyingi katikati mwa mji wakati dereva wake alipojaribu kuwakimbia watu waliokuwa wakitaka kuliharibu gari hilo.

Uganda Festnahme Robert Kyagulanyi aka Bobi Wine
Ni polisi na mfuasi wa Bobi WinePicha: Abubaker Lubowa/REUTERS

Picha kadhaa za machafuko hayo zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii zilionyesha kuwa hali ya taharuki ilikuwa imetanda kote. Rabsha aidha zilizuka mjini Gulu Kaskazini mwa Uganda wakati polisi walipomkamata mgombea wa chama kikuu cha upinzani cha FDC Patrick Oboi Amuriat lakini akaachiwa usiku wa kuamkia leo.

Hata hivyo hadi wakati wa kuandaa taarifa hii Bobi Wine alikuwa bado amezuiliwa katika korokoro ya polisi mjini Jinja chini ya ulinzi mkali na viongozi wa chama chake cha NUP hawajaruhusiwa kuonana naye. Katika mazingira haya, wagombea urais wawili majenerali Mugisha Muntu na Henry Tumukunde wametangaza kusitisha kampeni zao hadi pale Bobi Wine atakapoachiwa.

Licha ya baadhi ya shughuli za biashara kuanza tena mjini Kampala, bado kuna taharuki kutokana na doria kali sehemu mbalimbali za mji. Wengi wanaelezea kuwa hawawezi kutoka nyumbani hadi pale watakapojua hatima ya suala la kukamatwa kwa mgombea urais Bobi Wine ambaye amejitokeza kuwa mshindani mkuu dhidi ya rais Yoweri Museveni katika uchaguzi wa safari hii.