Watu 66 wauwawa nchini Syria
30 Januari 2012Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Ujerumani Guido Westerwelle jana ameanza ziara yake huko Mashariki ya Kati. Kituo cha kwanza katika ziara yake hiyo ya siku tano kilikuwa Amman, ambapo alielezea wito wa Ujerumani wa kutaka jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua za pamoja kukomesha machafuko nchini Syria.
Ujerumani ni miongoni mwa nchi wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambao waliwasilisha rasimu ya maazimo yao kuhusu Syria ijumaa. Urusi, yenye kura ya turufu, imesema haitaunga mkono rasimu ya hali yake sasa.
Baada ya mkutano wake na waziri mwenziwe wa mambo ya nje wa Jordan, Westerwelle alitoa wito pia kwa Wapalestina na Waisreal kurejea katika meza ya mazungumzo. Waziri huyo wa mambo ya nje wa Ujerumani anatarajiwa kwenda Misri, kabla kutembelea pia himaya za Palestina na Isreal.
Katika hatua nyingine nchini Syria vikosi vya Rais Bashar al-Assad vimefanya mashambulizi makubwa katika vitongoji vinavyodhibitiwa na waasi mjini Damascus. Makundi ya haki za binadamu yanasema watu 66 wameuwawa wakiwemo raia 26.