1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 58 wafariki katika mkasa wa moto London

Sekione Kitojo
18 Juni 2017

Polisi mjini London Jumamosi imepandisha idadi ya watu waliofariki na kufikia watu 58 ambao wamethibitishwa kufariki ama wanafikiriwa wamefariki kufuatia moto uliozuka katika jengo refu la mjini London la Grenfell Tower.

https://p.dw.com/p/2escb
UK Grenfell Tower in London
Jengo la Grenfell Tower mjini London Picha: picture alliance/AP Photo/F. Augstein

Ghadhabu  ya  umma  inaongezeka  wakati wakaazi  na  majirani wanadai  majibu  kuhusu  kwa  nini  moto huo uliozuka  mapema alfajiri  siku  ya  Jumatano  ulisambaa  haraka  na  kuwanasa  watu wengi  wakaazi  wapatao 600 wa  jengo  hilo . Vyombo  vya  habari nchini  Uingereza  vimeripoti kwamba  wakandarasi  waliweka vifaa hafifu, ambavyo havizuwii moto  katika kuta za  nje  za  jengo  hilo lenye ghorofa 24  katika ukarabati  ambao  ulimalizika mwaka  jana tu.

London Hochhausruine nach Brand
Waokoaji wakijaribu kusaka miili ya watu katika jengo la Grenfell Tower mjini LondonPicha: picture-alliance/dpa/PA/Wire/R. Findler

Kamanda  wa  polisi  Stuart Cundy  alisema  idadi  ya  watu  58 waliofariki  inatokana  na  ripoti  kutoka  kwa  umma  na  huenda ikaongezeka. Inajumuisha  watu 30  waliofariki ambao  tayari wamethibitishwa, na  ripoti  za  watu ambao  bado  hawajulikani waliko na  wanaaminika  kwamba  wamefariki. Amesema  itachukua wiki  kadhaa  ama  hata  zaidi  kuwapata  na  kuwatambua  wote waliofariki katika  jengo  hilo.

"Bahati  mbaya, katika  wakati  huu  kuna  watu 58 ambao wameelezwa  kwamba  walikuwamo  katika  jengo  hilo la  Grenfell Tower  katika  usiku huo  ambao  hawajulikani  waliko. Na  kwa  hiyo , kwa  masikitiko, nataka niamini  kwamba  wamefariki," alisema.

Amesema  polisi watatafakari kuchukua  hatua  za  kihalifu  iwapo kutakuwa  na  ushahidi  wa  makosa  na  kwamba  uchunguzi  wa polisi  utajumuisha  uchunguzi wa  mradi  huo  wa  ukarabati katika jengo  hilo, ambao  wataalamu  wanaamini  umesababisha   jengo hilo  kuwa  katika  hali mbya  ya  kukabiliwa  na  maafa  ya  moto.

UK Hochhausbrand in London - Hilfe von Nachbarn
Watu waliojitolea wakigawa misaada kwa watu walionusurika katika ajali ya moto mjini LondonPicha: Reuters/P. Hackett

Polisi  wamepata  shida  ya  kupata  idadi rasmi ya  nani  alikuwa katika  jengo  hilo wakati  moto  ulipozuka, na  kufanya  kuwa  vigumu kutambua  ni  watu  wangapi  wamefariki.

Watu wengi hawajulikani waliko

Cundy  amesema huenda  kulikuwa  na  watu  wengine  katika  jengo hilo  ambao polisi  haina  habari  nao, na  kwamba  inaweza kuongeza  idadi  ya  vifo. Amemtaka  kila  mtu ambaye  alikuwa katika  jengo  hilo na  ambaye  amenusurika kuwasiliana  na  polisi mara  moja.

Polisi  imesema  msako wa  mabaki  ya  miili  ya   watu ulisita  siku ya  Ijumaa kutokana  na  wasi  wasi  wa  usalama katika  jengo  hilo lililoungua  moto lakini  sasa  zoezi  hilo  limeanza  tena. Cundy amesema  wafanyakazi  wa  kutoa  huduma  ya  dharura sasa  wamefikia  juu  kabisa  mwa  jengo  hilo.

Waziri  mkuu  wa  Uingereza  Theresa May , akikabiliwa  na  ukosoaji kwa  jinsi  serikali  ilivyoshughulikia  maafa  hayo, alikutana  jana Jumamosi (17.06.2017)na watu 15 walionusurika  katika  moto waliokaribishwa ofisini  kwake mtaa  wa Downing  namba 10. Kundi hilo  liliondoka  baada  ya  mkutano  ambao  ulidumu  kwa  zaidi  ya masaa  mawili  lakini  hawakuzungumza  na  waandishi  habari waliokusanyika  nje ya  ofisi  hiyo.

Mkutano  huo  huenda  utatuliza  malalamiko kwamba  May amekuwa taratibu  mno  kuwawafikia  watu walionusurika, licha  ya kutangaza mfuko wa  dola milioni 6.4 wa  dharura  kuwasaidia familia ambazo hazina  makaazi.

Mwandishi: Sekione Kitojo / ape

Mhariri: Sudi Mnette