1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 33 wauawa kwa bomu Irak.

Halima Nyanza3 Machi 2010

Watu 33 wameuawa na wengine 55 wamejeruhiwa katika mashambulio matatu ya kujitoa mhanga yaliyotokea Katika mji wa Ba'quba nchini Iraq, ikiwa ni siku chache tu kabla ya kufanyika uchaguzi mkuu nchini humo.

https://p.dw.com/p/MIsq
Mwanajeshi wa Irak, wakipiga doria katika mji wa Basra. licha ya ulinzi uliowekwa, watu 33 wameuawa katika mashambulio ya bomu ya kujitoa mhanga yaliyotokea mapema leo.Picha: AP

Mashambulio hayo, likiwemo lile ambalo lilifanywa na mshambuliaji aliyejiripua ndani ya gari la wagonjwa alilokuwa amepanda wakati likielekea hospitali, yamesababisha vifo vya watu wengi zaidi katika kipindi cha karibu mwezi sasa. Pia yamesababisha majeshi ya usalama nchini Iraq kushinikiza haraka kuwekwa amri ya watu kutotembea ovyo katika mji huo wa Ba'quba ulioko kilomita 60 kaskazini mwa mji mkuu wa Baghdad.

Duru za usalama nchini humo zinasema kuwa miongoni mwa watu hao waliokufa ni polisi 10.

Duru hizo zimeeleza kuwa mabomu mawili yaliyoripuka kwa wakati mmoja yaliyokuwa yametegeshwa katika gari, yalishambulia jengo la ofisi ya jimbo hilo la Diyala, na katika njia panda iliyopo katika eneo hilo. Ofisi hizo pia zipo karibu na kituo cha polisi.

Akizungumzia tukio lingine, msemaji wa polisi wa Ba'quba, Meja Ghaleb al Juburi, amesema mshambuliaji aliyekuwa amevalia nguo za polisi aliingia na majeruhi katika gari la wagonjwa lililokuwa likielekea hospitali na kisha kujiripua.

Habari zinasema pia mshambuliaji huyo wa kujitoa mhanga alipanga kujiripua, wakati kamanda wa polisi, Meja Generali Abdul Hussein al Shimmari, akija kuwajulia hali majeruhi hospitalini hapo.

Hata hivyo, mkuu huyo wa polisi alifanikiwa kunusurika, lakini walinzi wake walijeruhiwa.

Miongoni mwa waliojeruhiwa katika shambulio hilo ni pamoja na Mkuu wa kitengo cha afya wa jimbo hilo la Diyala.

Mashambulio hayo yamefanyika licha ya ulinzi mkali uliowekwa nchi nzima kuelekea uchaguzi mkuu wa Jumapili, baada ya kiongozi wa Al Qaeda nchini Iraq, Abu Omar al Baghdadi, kutishia kuuvuruga uchaguzi huo.

Mshauri wa Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Nuri al Maliki, Ali al-Mussawi, amedai kuwa mashambulio hayo ni ya kigaidi ambayo yamepangwa kuvuruga zoezi hilo la upigaji kura linalotarajiwa kufanyika Jumapili ya wiki hii.

Amesema kuwa mashambulio hayo yamefanywa ili kuwafanya watu wachanganyikiwe na kuwafanya wasiende kupiga kura kutokana na kwamba uchaguzi ni tishio kubwa kwa magaidi.

Shambulio hilo la leo linaongoza kwa kusababisha vifo vya watu wengi nchini humo tangu Februari tano, ambapo mahujaji 41 wa Kishia waliuawa katika mji mtakatifu wa Karbala.

Ba'quba, ambao ni mji mkuu wa jimbo la Diyala, ulikuwa ni mahala pa wapiganaji wa Kisunni, wakati majeshi ya Marekani yalipoivamia nchi hiyo mwaka 2003.

Siku ya Jumapili, mwishoni mwa wiki hii, Wairaqi wanapiga kura kuchagua bunge la nchi hiyo, uchaguzi ambao ni wa pili kufanyika toka aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Saddam Hussein, kuondolewa madarakani mwaka 2003.

Mwandishi: Halima Nyanza(afp)

Mhariri: Othman, Miraji