Watu 100 wauawa katika mapigano Yemen | Matukio ya Kisiasa | DW | 20.02.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Watu 100 wauawa katika mapigano Yemen

Kulingana na ripoti ya jeshi la Yemen, katika siku tano zilizopita zaidi ya watu 100 waliuawa katika mapigano kati ya jeshi la serikali na waasi wa Kishia. Mapigano haya yanaendelea Kaskazini mwa nchi hiyo.

Rais Ali Abdullah Saleh wa Yemen

Rais Ali Abdullah Saleh wa Yemen

Kama msemaji wa jeshi alivyoarifu jana usiku, 90 kati ya waliouawa ni wanajeshi wa serikali. Jeshi lilitumia mizinga mikubwa kushambulia maeneo ya Saada, kilomita 180 hivi Kaskazini mwa mji mkuu wa Yemen, San'a, karibu na mpaka na Saudi Arabia ambako waasi wa Kishia wanaaminika kujificha. Katika wiki kadhaa zilizopita maafisa 200 hivi wa jeshi na polisi ya Yemen waliuawa. Hakuna ripoti rasmi juu ya idadi ya waasi waliouawa, lakini kulingana na viongozi wa kikabila zaidi ya waasi 100 waliuwawa katika mapigano haya yaliyozuka tena mwisho mwa mwezi wa Januari.

Jumamosi iliyopita, rais wa Yemen, Ali Abdullah Saleh aliwapa waasi hawa muda wa siku mbili kuweka chini silaha zao na kulivunja kundi lao ama sivyo wataangamizwa. Ikiwa lakini wataitikia wito huo, rais atawaruhusu kuunda chama cha kisiasa lakini msingi wake usiwe wa kikabila.

Kiongozi wa waasi hawa wanaojulikana kama “Believing Youth” - “Vijana wanaoamini” ni Abdul-Malik al-Houthi, ambaye ni kaka wa kiongozi wa zamani, Hussein Badr Eddin al-Houthi. Huyu alianzisha uasi huo mwezi wa Juni 2004 lakini aliuawa miezi mitatu baada ya hapo katika mapigano na jeshi la serikali. Waasi hawa wanailaumu serikali kwa rushwa na kuwa na mahusiano ya karibu na nchi za Magharibi.

Rais Ali Abdullah aliwashutumu waasi kuwa wasaliti waliojiuza , ili kuliathiri taifa la Yemen na maslahi yake. Pia alisema, wafuasi wa Houthi wanajaribu kuiangusha serikali yake ya jamhuri na kuweka mfumo wa kiislamu wakiungwa mkono na na makundi kutoka nje. Ripoti nyingine za vyombo vya habari ziliwanukuu maafisa wa serikali wakisishutumu Iran na Libya kwa kuwasaidia kifedha waasi hawa. Katika mahojiano yaliyochapishwa katika gazeti moja la Yemen, kiongozi wa waasi Abdel Malek al-Hauthi alikanusha kuwa na uhusiano wowote na nchi hizo na aliishutumu serikali kwa kutaka kumaliza mzozo huu kwa kutumia silaha badala ya mazungumzo.

 • Tarehe 20.02.2007
 • Mwandishi Maja Dreyer
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CHJq
 • Tarehe 20.02.2007
 • Mwandishi Maja Dreyer
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CHJq

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com