1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanasheria wanasema zuio jipya lina nguvu mahakamani

27 Septemba 2017

Katika zuio la sasa, nchi tatu zimeongezwa ambazo ni Venezuela, Chad na Korea Kaskazini

https://p.dw.com/p/2kpaR
Donald Trump
Picha: picture-alliance/AP Photo/B. Anderson

Wakati tangazo jipya la Rais wa Marekani, Donald Trump, la kuzuia wageni kutoka nchi kadhaa  zikiwamo za kiislamu kuingia Marekani, likikosolewa kwa kiasi kikubwa,  kwa upande mwingine wataalamu wameonya kuwa  zuio la sasa  linaweza kuwa na nguvu mahakamani.

Hili ni zuio la pili baada ya lile la  Machi mwaka huu, ambapo Trump alizuia raia wa  nchi sita za kiislamu  ikiwamo Iran, Libya, Syria, Yemen, Somalia na Sudan.  Lakini zuio alilolitoa Jumapili limeongeza nchi nyingine tatu ikiwamo Korea Kaskazini, Chad na baadhi ya maofisa wa serikali kutoka Venezuela.

Hata hivyo, zuio hili jipya kama ilivyokuwa kwa la awali, limekosolewa vikali na watetezi wa haki za binadamu na taasisi zinazohudumia wakimbizi.

Wataalamu wa sheria na wasomi hata hivyo wamesema zuio hilo, linalotarajiwa kuanza kufanya kazi Oktoba 18 mwaka huu  huenda lisiathiriwe sana  na mashambulizi ya kisheria.  Wamesema zuio hilo ni  matokeo ya miezi kadhaa ya uchambuzi  na uchunguzi  uliofanywa na  maofisa wa Marekani.  Pia zuio hilo linatajwa kuwa huenda halihusiani na  kauli za Trump alizozitoa wakati wa kampeni zake ambazo baadhi ya mahakama iliziona kama ni za kibaguzi dhidi ya waislamu.

Profesa wa Chuo Kikuu cha Virginia, Shulen ya Sheria, Saikrishna Prakash amesema suala la sasa linaonekana halihusiani na  sababu yoyote  binafsi au kutimiza ahadi zake za wakati wa kampeni.

 Serikali imesema, Rais ana mamlaka makubwa katika masuala ya uhamiaji na ya usalama wa taifa, lakini wakosoaji wa zuio la Machi, walihoji na kusema zuio hilo linaiweka Marekani katrika matatizo. Kadhalika walinukuu kauli ya Trump aliyoitoa wakati wa kampeni zake mwaka 2016, aliposema kuwa atazuia kabisa waislamu kuingia Marekani.

 Serikali ya Marekani ilifanya tathmini katika nchi kabla ya zuio la pili

 Saa chache tu baada ya zuio la juzi, wanasheria wanaowakilisha maeneo   ya  Hawaii, New York na California, walisema wameanza kupitia zuio jipya. Taasisi za utetezi nazo zilisema zinafanya hivyo.

 Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mradi wa Kimataifa wa kuwasaidia wakimbizi, Becca Heller, alisema bado ni zuio la waislamu isipokuwa tu limeongeza nchi tatu.

``Kati ya nchi hizo, Chad ndiyo yenye idadi kubwa ya waislamu, safari za  Korea Kaskazini,  zilishapungua na zuio kwa Venezuela litawaathiri maofisa kadhaa wa serikali katika visa fulani tu,`` anasema Heller

US Einreiseverbot Protest
Picha: Getty Images/D. Angerer

 Lakini tathmini  iliyofanywa dunia nzima na zuio jipya katika nchi hizo inaweza kuzidhoofisha hoja za wataalamu na wanasheria wanaolipina mahakamani.

 Tathmini hiyo imechunguza uwezo wa nchi kutoa hati ya kusafiria kwa njia ya kielektroniki na nchi hizo kushirikishana taarifa za hali  ya usalama  na  Marekani.

 Taarifa ya Trump imesema baada ya tathmini hiyo kufanywa,  kwa ujumla nchi 47 zilionekana kuwa na shida, na 40 zilifanya marekebisho zikiwamo 11 ambazo zilikubali kushirikishana taarifa kuhusu ugaidi.

Wakati hayo yakijiri, Mahakama Kuu ya Marekani imesema haitaendelea tena na kesi kuhusu  zuio la Machi mwaka huu baada ya zuio jipya kutolewa . Awali  Mahakama hiyo ilipanga kusikiliza madai hayo ya  zuio la wasafiri  wa nchi za Kiislamu, mnamo Oktoba 10. 

 Wakati huo huo, wataalamu wamesema licha ya kuwa  madai mapya ya unyanyapaa wa kidini yanaweza kukosa mashiko, lakini wakosoaji wanaweza kuleta hoja kuwa zuio hilo linakiuka Sheria za Uhamiaji na Utaifa ambayo inazuia serikali kunyanyapaa utaifa wa mtu wakati inapotoa  visa.

 Mwandishi: Florence Majani

Mhariri:  Josephat Charo