Wasoshialisti waondolewa patupu Ufaransa
31 Machi 2014"Rais amevuliwa nguo" ndio kichwa cha maneno cha gazeti la mrengo wa shoto La Liberation linalohisi rais Hollande ambae hapendi kupitisha uamuzi kwa pupa,hawezi tena kukwepa na "anabidi afichue haraka kile anachodhamiria kufanya."
"Zilzala,pigo,adhabu,hatakiwi" ni miongoni mwa vichwa vya maneno katika magazeti ya Ufaransa yanayotoa picha ya janga linalomgubika rais Hollande baada ya uchaguzi huu ambao ni wa kwanza tangu aingie madarakani mwezi Mai mwaka 2012.
Kambi ya wasoshialisti imepokonywa na wahafidhina miji isiyopungua 155 yenye wakaazi zaidi ya 9000-na baadhi ya miji hiyo ilikuwa ikiongozwa na mrengo wa shoto kwa zaidi ya miaka 100.
Sauti zinazidi kupazwa waziri mkuu abadilishwe
Miito kutaka waziri mkuu abadilishwe imezidi kupata nguvu sio tu kutoka kambi ya wahafidhina bali pia mrengo wa shoto. Jean-Marc Ayrault anatwikwa jukumu la kushindwa siasa ya serikali ya Ufaransa tangu takriban miaka miwili iliyopita.Kwa mujibu wa utafiti wa maoni ya wananchi uliosimamiwa na taasisi ya BVA,zaidi ya robo tatu ya wafaransa wasingependelea kumuona Jean Marc Ayrault akiendelea kuongoza serikali.
Wakaribu wa rais Francois Hollande wamesema wazi jana usiku "ujumbe wameupata".Rais Francois Hollande anatazamiwa kulihutubia taifa leo hii."Wapiga kura wameelezea hisia zao...na baadhi ya wakati kwa hasira" amesema hayo waziri wa mambo ya ndani Manuel Valls anaepewa nafasi nzuri ya kuteuliwa kuwa waziri mkuu mpya.Amekiri matokeo ya uchaguzi wa jana ni pigo kwa chama cha kishoshiliasti tangu katika daraja ya kimkoa mpaka kitaifa.
Manuel Valls alikuwa akutane na rais Francois Hollande leo asubuhi kabla ya rais Hollande kuzungumza na waziri mkuu Jean-Marc Ayrault.
Jean Marc Ayrault ameungama anabeba shemu ya dhamana ya pigo hilo linaloashiria na mengine yanaweza kufuata mfano katika uchaguzi wa bunge la ulaya mwezi May ujao na ule wa baraza la senet ambao unaweza kupibndua wizanio wa nguvu na kuelemea mrengo wa kulia.
Nukhsii inaiandama serikali ya kisoshialiti
Pigo la uchaguzi limechanganyika na ripoti zilizochapishwa leo kuhusu kuongezeka nakisi ya bajeti ya nchi hiyo.Katika wakati ambapo lengo lilikuwa kuipunguza hadi asili mia 4.1 ya pato la ndani kwa mwaka 2013 dhidi ya asili mia 4.9 mwaka 2012,nakisi hiyo imefikia asili mia 4.3.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Reuters/AFP
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman