Washtakiwa uhalifu wa vitani Darfur wakamatwe | Matukio ya Kisiasa | DW | 08.06.2007
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Washtakiwa uhalifu wa vitani Darfur wakamatwe

Mahakama ya Uhalifu ya Kimataifa-(ICC)imetoa mwito kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuishinikiza Sudan kuwakamata watuhumiwa wawili walioshtakiwa uhalifu wa vitani katika jimbo la Darfur.

Wakimbizi wa Darfur wangojea misaada kwenye kambi ya Abou Shouk

Wakimbizi wa Darfur wangojea misaada kwenye kambi ya Abou Shouk

Mwendesha mashtaka mkuu wa Mahakama ya Uhalifu ya Kimataifa,Luis Moreno-Ocampo alipozungumza mjini New York katika Umoja wa Mataifa alisema,aliekuwa waziri wa ndani wa Sudan,Ahmad Harun na kiongozi wa wanamgambo Ali Kushayb,wanaoshtakiwa mauaji ya halaiki,ubakaji na kuwafukuza kwa nguvu maelefu ya watu kutoka majumbani mwao,wanapaswa kukamatwa na serikali ya Sudan na kufikishwa katika mahakama ya kimataifa.Lakini hilo si rahisi, kwani Khartoum mara kwa mara imesema,watuhumiwa hao,hawatopelekwa mbele ya mahakama hiyo na hakuna jeshi litakalokwenda Sudan kuwakamata.

Lakini Moreno-Ocampo amesema:

“Ahmad Harun kama waziri wa ndani alihusika na vitendo vya ukatili mkubwa dhidi ya umma na watu hao kufukuzwa makwao.Na leo,yeye ni waziri wa shughuli za kiutu.Watu waliokuwa wahanga wake, sasa wamo mikononi mwake,hilo halikubaliki.“

Wakati huo huo,balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Zalmay Khalilzad alisema,pindi Sudan haitokubali kwa haraka,basi Baraza la Usalama litapendekeza vikwazo zaidi vya kimataifa dhidi ya Sudan.

Lakini China,kwa mara nyingine tena imeonya vikali dhidi ya kuishinikiza na kuiwekea Sudan vikwazo zaidi kuhusika na suala la Darfur.

Juu ya hivyo nchini Marekani,sauti zinazidi kupazwa ikitolewa mito ya kutafuta suluhisho la mgogoro wa Darfur.Bill Richardson,balozi wa zamani wa Marekani katika Umoja wa Mataifa na anaetaka kugombea urais kwa tikti ya chama cha Demokrats,amesema:

„Tunaihitaji China,iliyo na ushawishi mkubwa katika Darfur na ikiwa haitaki kufanya lo lolote, basi sisi labda tusiende kwenye michezo ya Olimpics.“

China kwa upande wake imesema,ni kosa kulifungamanisha suala la Darfur na michezo ya Olimpics ya majira ya joto itakayofanywa China mwaka ujao.China,hununua theluthi mbili ya mauzo ya mafuta ya Sudan na vile vile huiuzia Sudan silaha na ndege za kijeshi.Juhudi za kutaka kupeleka Darfur vikosi vya amani vya Umoja wa Mataifa bila ya idhini ya Sudan,zimepingwa na China iliyo na kura ya turufu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com