1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Washington: Wamarekani wanakataa kuwakabidhi mashushushu wao kwa Italy

28 Februari 2007
https://p.dw.com/p/CCNn

Mshauri wa kisheria wa wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani amesema nchi yake haitaikubalia Italy warejeshwe nchini humo mashushushu wa shirika la ujasusi la Marekani, CIA, ambao wametajwa kwamba wanatuhumiwa kumteka nyara shehe wa Kimisri mjini Milan. John Bellinger alitoa taarifa hiyo baada ya kukutana na washauri wa kisheria wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels. Waendeshaji wa mashtaka wa Kitaliana huko Milan wanaitaka serekali ya nchi yao iwasilishe ombi lao kwa serekali ya Marekani ili kwamba Wamarekani 26, wengi wao wakiwa ni mashushushu wa shirika la ujasusi la CIA, warejeshwe Milan. Wamarekani hao 26 wanatuhumiwa walimteka nyara Osama Moustafa Hassan Nasr kutoka barabara ya Milan hapo Februari, mwaka 2003, na baadae kumsafirisha kwa ndege hadi Misri. Huko Nasr alishikiliwa kwa miaka minne. Kwa mujibu wa wakili wake, ni kwamba aliteswa. Aliachiliwa huru wiki iliopita na mahakama ya Misri ambayo ilisema kuwekwa kwake kizuizini kulikuwa hakuna msingi.