1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Warepublican washinda katika Jimbo la Georgia

Caro Robi
21 Juni 2017

Mgombea wa chama cha Republican Karen Handel ameshinda uchaguzi maalumu wa bunge uliokuwa na ushindani mkali na uliokuwa ukifuatliwa kwa karibu katika jimbo la Georgia nchini Marekani.

https://p.dw.com/p/2f4d3
USA Wahlen in Georgia
Picha: Reuters/C. Aluka Berry

Handel, kigogo wa Republican na waziri wa zamani wa mambo ya nje wa jimbo la Georgia amemshinda mpinzani wake Mdemocrat Jon Ossoff asiye na uzoefu wa siasa kwa takriban asilimia 52 dhidi ya 48 ya kura na hivyo kukinyima chama cha Democratic ushindi wao wa kwanza mwaka huu.

Akikubali kushindwa, Ossof amesema wanachama cha chama cha Democratic wanapaswa kujifunza kutoka kwa chaguzi hizo na kujiandaa vyema katika kinyanganyiro kikubwa cha kulidhibiti bunge mwaka ujao.

Ushindi pigo kwa Wademocrat

Ushindi huo wa Handel umekiuka ubashiri wa kura za maoni zilizoonesha Handel alikuwa nyuma ya Ossof kabla ya uchaguzi huo na hivyo basi unaashiria, kinyume na matarajio ya Wademocrats kuwa wapiga kura wa Republican wamevunjwa moyo na utawala wa Trump, wangemuunga mkono mgombea wao, lakini hilo halikuwa.

USA Karen Handel
Karen Handel aliyeshinda uchaguziPicha: picture alliance/AP Photo/D. Goldman

Trump ambaye aliwaomba wapiga kura kumininika katika vituo vya kupigia kura katika eneo la uwakilishi la Georgia sixth ametumia ukurasa wake wa Twitter kumpongeza Handel kwa kunyakua ushindi.

Ushindi huo bila shaka ni afueni kwa Warepublican ambao wamekuwa na wasiwasi kuwa kutokana na misururu ya kashfa zinazoukumba utawala wa Trump, wangeweza kukishida kiti hicho cha Georgia sixth ambacho kimekuwa kinyang'anyiro kilichogharimu zaidi katika historia ya Marekani.

Kiasi ya dola milioni 57 zilitumika katika uchaguzi huo. Warepublican wamekuwa wakilitawala eneo hilo tangu 1979.

Trump ajipiga kifua Twitter

Mwenyekiti wa kitaifa wa chama cha Republican Ronna McDaniel amesema watu wa eneo bunge la Georgia Sixth wamempigia kura kwa wingi sio tu Karen Handel, bali pia ajenda za Rais Trump za kubadilisha mfumo wa bima ya afya, kubadilisha mfumo wa kodi uliopitwa na wakati na kuupa kipaumbele uwekezaji wa miundo mbinu.

USA Donald Trump steigt in die Air Force One
Rais wa Marekani Donald TrumpPicha: Reuters/J. Ernst

Chama cha Trump pia kilishinda katika uchaguzi mwingine wa bunge jana, katika jimbo jirani la South Carolina. Viti hivyo viwili vilibaki wazi baada ya wabunge waliokuwa wamechaguliwa katika uchaguzi mkuu katika maeneo hayo, kujiunga na baraza la mawaziri la Trump.

Wagombea wa Democratic awali pia walipoteza katika chaguzi zilizofanyika katika ngome za Warepublican za Kansas na Montana. Ushindi huo ulimpa fursa Trump kujipiga kifua akiandika Twitter kuwa chaguzi maalumu zimekwisha na wanaotaka kuifanya Marekani imara tena wameshinda tano bila, na habari zote za uongo pamoja na pesa zote zilizotumika wameambulia patupu!

Upinzani ulikuwa una nadi sera za kuwa chaguzi hizo ni kura ya maoni kwa utawala wa Trump uliozongwa na kashfa moja baada ya nyingine.

Mwandishi: Caro Robi/afp/Reuters

Mhariri:Josephat Charo