1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wapinzani watishia kususia bunge Algeria

Admin.WagnerD14 Mei 2012

Kiongozi wa chama cha Kiislamu nchini Algeria, Abdallah Djaballah, ametishia kuhamasisha vyama vidogo kufanya mandamano kupinga matokeo ya uchaguzi wa wabunge nchini humo.

https://p.dw.com/p/14vDs
Abdallah Djaballah
Abdallah DjaballahPicha: AP

Djaballah amesema matokeo hayo yaliyokipa ushindi mkubwa chama tawala cha rais Abdul Aziz Bouteflika yamefunga mlango wa mabadiliko na njia iliyobaki ni kuingia mitaani kama ilivyofanyika huko Tunisia.

Kwa mujibu wa matokeo ya mwanzo, chama cha Djaballah cha Front for Justice and Develeopment kiliambulia viti 7 tu kati ya 462 vilivyogombaniwa katika uchaguzi wa Alhamis wiki iliyopita, ambao pia ulisifiwa na Marekani kama mwanzo mpya wa kuelekea demokrasia ya kweli nchini Algeria.

Chama cha rais Abdul Aziz Boutefilika, cha National Liberation Front ambacho kimeitawala Algeria tangu ilipopata uhuru miaka 50 iliyopita, kimejizatiti kwa kupata jumla ya viti 220. Matokeo rasmi yalitarajiwa kutolewa Jumatatu jioni.

Rais wa Algeria Abdelaziz Bouteflika akipiga kura katika uchaguzi huo.
Rais wa Algeria Abdelaziz Bouteflika akipiga kura katika uchaguzi huo.Picha: Reuters

Matumaini yaliyofifia
Djballah alitarajia kunufaika na athari za mageuzi yaliyofanyika katika mataifa ya kiarabu kwa kupata ushindi kama vilivyoupata vyama vinavyoegemea dini katika mataifa kadhaa ya kiarabu, lakini haikuwa hivyo, na badala yake vyama vya Kiislamu vimejikuta vikianguka vibaya kwa kupata jumla ya viti 59 tu.

Djaballah, mwenye umri wa miaka 56, alitahadharisha mapema juu ya kuwepo njama za wizi wa kura na kudai kuwa chama chake kingeibuka na ushindi hata kama uchaguzi huu ungefanyika kwa uwazi kwa asilimia 80. Alidai kuwa na nyaraka zinazothibitisha kuwa kura za maoni zilizoendeshwa na serikali zilionyesha chama chake cha FJD kingeshinda viti 65.

Vyama vidogo vilivyopata viti 20 au chini yake, vimesema kura ziliibwa mwanzo hadi mwisho, madai ambayo yanaungwa mkono na wa waalgeria wengi na wachambuzi pia

Kupeleka malalamiko mahakama ya katiba
Chama cha Wafanyakazi, kile cha kisoshalisti, cha Algerian National Front na vingine, vyote vimedai kuibiwa kura zake na vimetishia kupinga matokeo hayo katika mahakama ya katiba. Djaballah amesema wanafanya majadiliano na vyama vyote hivyo ili kuwa na msimamo mmoja. Ameongoza kuwa kama vyama hivyo vitakubaliana kususia Bunge, basi chama chake ndiyo kitakuwa cha kwanza kutangaza uamuzi huo.

Waziri wa Mambo ya ndani wa Algeria Daho Ould Kablia akitangaza matokeo ya uchaguzi.
Waziri wa Mambo ya ndani wa Algeria Daho Ould Kablia akitangaza matokeo ya uchaguzi.Picha: Reuters

Djaballah, ambaye amewahi kugombea urais wa nchi hiyo mara mbili, anasimama katikati ya chama kilichopigwa marufuku cha Islamic Salvation Front kilichopambana na serikali wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe, na tawi la chama cha Udugu wa Kiislamu ambao ni washirika katika Serikali ya rais Boutefilika.

Wakati huo huo, mahakama moja nchini humo imemhukumu kwenda jela miezi sita, Sheikh Jamil Salwi ambaye ni Msalafi kutokea Yemeni kwa kosa la kutoa mawaidha dhidi ya upigaji kura. Mahakama hiyo pia imemtoza faini ya dola 1,300 na kumpiga marufuku kuingia nchini humo kwa muda wa miaka 10.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga\AFPE
Mhariri: Othman Miraji