1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanajeshi wa Uengereza waihama Basra

Oummilkheir3 Septemba 2007

Wanajeshi wa Uengereza wameuhama mji wa Basra hii leo na kuwakabidhi wanajeshi wa Irak hatamu za uongozi wa jiji hilo kubwa la kusini. Waziri mkuu Gordon Brown amesema opereshini hiyo iliyoanza jana iliandaliwa tangu zamani.

https://p.dw.com/p/CB1Z
Bendera ya Irak yapepea Basra
Bendera ya Irak yapepea BasraPicha: AP

“Wanajeshi 500 wa Uengereza wameshalihama kasri walilokua wakilitumia kama makao makuu yao mjini Basra,kabla ya alfajiri ya leo-“,amesema hayo,jenerali Mohan Fahed, mkuu wa opereshini za kijeshi katika mji huo ulioko umbali wa kilomita 550 kusini mwa Baghdad.

Wakipiga kambi tangu March mwaka 2003 katika mji huo wa Basra wanakoishi wairak wengi wa madhehebu ya shiya,wanajeshi wa Uengereza wamehamia katika ngome ya jeshi la wanaanga,karibu na uwanja wa ndege umbali wa kilomita 25 toka Basra,wakijiunga na wenzao elfu tano wanaowapatia mafunzo wanajeshi wa Iraki.

Msemaji wa jeshi la Uengereza mjini Basra,kamanda Mike Shearer amesema ripoti rasmi itatangazwa “mara tuu opereshini itakapokamilika.”

“Wanajeshi wa Uengereza wameanza kuihama kasri ya Basra tangu saa tano za usiku jana”-amesema jenerali Mohan Fahed,aliyeongeza kusema tunanukuu:”Jeshi la Irak linaidhibiti hali ya mambo katika eneo hilo ambalo ni marufuku kuanzia sasa. Hakuna anaeruhusiwa kukurubia eneo hilo,hadi waziri mkuu Nouri el Maliki atakapoamua hatima ya kasri hilo.”

Kasri hilo la fahari lililokua likikaliwa na wanajeshi wa Uengereza liliundwa na rais wa zamani Sadam Hussein katika ujia wa maji wa Chaat el Arab-unaoitenganisha Iran na Irak.

Wanajeshi wa Uengereza wameuhama mji wa Basra licha ya kukasirika wamarekani katika wakati ambapo uhusiano kati ya washirika hawa wawili unazidi kulega lega.

Mwishoni mwa mwezi uliopita,wizara ya ulinzi ya Marekani-Pentagone,ilizungumzia “hofu”,pindi wanajeshi wa Uengereza wataondoka Basra ambako hali ni ya mparaganyiko, na makundi ya wahalifu yanahatarisha usalama.”

Malcon Rifkind,aliyewahi kua waziri wa mambo ya nchi za nje wa Uengereza anasema: “Ingekua serikali ya Uengereza imeweka wazi kabisa kwamba hairidhishwi na sera za rais George W. Bush zilizokua zikitekelezwa na Rumsfeld,basi sera hizo zingebadilishwa,na kwa namna hiyo wanajeshi wachache wa Marekani wangeuwawa, maisha ya wanajeshi wachache pia wa Uengereza yangeteketea na pia raia wachache wa Irak wangepoteza maisha yao-katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.”

Majenerali kadhaa wa zamani wa Uengereza wamekua pia wakikosoa hadharani mkakati wa kijeshi unaofuatwa na Marekani nchini Irak tangu vita vilipomaliozika.

Wanajeshi 159 wa Uengereza wameuwawa tangu vikosi vya nchi shirika vinavyoongozwa na Marekani kuivamia Irak mwaka 2003.

Waziri mkuu wa Uengereza Gordon Brown amesema hii leo kuhamishwa wanajeshi wa nchi yake toka Basra ni opereshini iliyoandaliwa tangu zamani na haimaanishi wameshindwa.Kwa maoni yake, wanajeshi wa Uengereza wataendelea kuchangia ipasavyo na kuwapatia mafunzo wanajeshi wa Irak.