1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanajeshi wa baraza la mpito wateka bandari ya Sirte

27 Septemba 2011

Wanajeshi wa utawala mpya wa Libya wanaidhibiti bandari ya mji wa Sirte- ngome ya kiongozi wa zamani Muammar Gaddafi. Mamia ya watu wanaukimbia mji huo.

https://p.dw.com/p/12h5p
Mapigano yapamba moto SirtePicha: dapd

Mapigano yameanza jana usiku na hivi sasa tunaidhibiti bandari ya Sirte, amesema hayo Mustafa ben Dardef, mkuu wa kikosi cha Zenten cha baraza la mpito kilichowekwa karibu na mji wa Syrte.

Tutakapojongelea eneo la kati mapigano yataenea majiani na tunajiandaa kwa hali hiyo, amesema kwa upande wake Ali Saidi, ambae ni miongoni mwa wapiganaji, huku wenzake wakisafisha na kupaka mafuta silaha zao.

Mapigano yameripuka jana usiku karibu na bandari ya mji huo wa wakaazi 70 elfu, ulioko umbali wa kilomita 360 mashariki ya Tripoli ambao ulizungukwa na wapiganaji wa baraza la mpito wanaosonga mbele wakitokea mashariki na magharibi pia.

NATO Kampagne in Libyen
Kampeni ya NATO nchini LibyaPicha: DW

Kwa mujibu wa Umoja wa mataifa, watu elfu mbili wameupa kisogo mji huo ambao, kwa mujibu wa mashahidi, una ukosefu wa maji, umeme na chakula. Watoto ndio wanaotaabika zaidi. Katika hospitali ya Harawa iliyoko umbali wa kilomita 40 mashariki ya Sirte, dazeni za watoto wanapelekwa kila siku ,wakiugua maradhi yanayosababishwa na ukosefu wa maji safi.

Kwa mujibu wa mwanajeshi mmoja wa baraza la mpito, wanamgambo wawili wa kiongozi wa zamani wa Libya wamesalim amri jana usiku. "Wamejileta wenyewe na kutukabidhi silaha na magari yao",amesema Maatiz Saad aliyehakikisha mapigano bado yanaendelea.

Libyen Trümmer Ruinen Zliten 04.08.2011
Magofu ya nyumba nchini LibyaPicha: dapd

Jumuia ya kujihami ya NATO imesema ndege zake za kivita zimezidisha hujuma dhidi ya vituo kadhaa vya kijeshi huko Sirte.

Ripoti zinazidi kuongezeka kwamba mmojawapo wa watoto wa kiume wa Muammar Gaddafi, Mutassim anakutikana katika vitongoji vya kusini vya Sirte.

Wapiganaji wa baraza la mpito wanaamini mtoto maarufu wa Gaddafi, Seif al-Islam yuko katika mji mwengine unaodhibitiwa na wanamgambo wa Gaddafi-Bani Walid ambako mapigano pia yanaendelea.

Viongozi wa baraza la mpito wana hamu ya kumkamata Gaddafi ambae hakuna ajuae amejificha wapi na kumfikisha mahakamani pamoja na viongozi wengine wa utawala wake kwa tuhuma za kuvunja "vibaya sana haki za binaadam" wakati wa utawala wake wa miaka 42.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Afp/Reuters

Mhariri: Miraji Othman