1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Afrika

Wamisri wataka jeshi kuondoka madarakani

Wanaharakati wa haki za kibinaadamu wameitisha maandamano nchini Misri kushinikiza utawala wa kijeshi liondoke madarakani, na pia kulaani ghasia za kandanda katika mji wa Port Said.

Waandamanaji nchini Misri

Waandamanaji nchini Misri

Wanaharakati hao wamekasirishwa na vifo vya watu 74 vilivyotokea kati ya mashabiki wa soka wa vilabu viwili hasimu katika mji wa Port Said.

Maandamano hayo yanatarajiwa kuanza hii leo katika maeneo mbali mbali mjini Cairo baada ya sala ya ijumaa. Kulingana na taarifa iliotumwa katika mtandao kutoka kwa makundi 28 yanayopigania demokrasia nchini humo, wataandamana hadi katika bunge la nchi hiyo, kutaka baraza la jeshi ambalo lilichukua utawala kufuatia mapinduzi yaliomg'oa madarakani rais wa zamani Hosni Mubarak.

Wanaharakati, wanalishitumu baraza hilo la kijeshi kwa usimamizi mbaya katika kipindi hiki cha mpito nchini humo, na pia kulilaumu kwa ghasia za kandanda kati ya wafuasi wa timu ya Al Ahli na Al Masri zilizosababisha vifo vya watu 74, kaskazini mwa mji wa Port Said.

Ghasia hizo zilizotokea siku mbili zilizopita, zimesababisha maandamano mengine zaidi katika miji tofauti nchini Misri ambapo sasa yamezua mapambanao makali kati ya polisi na waandamanaji. Kulingana na wahudumu wa afya, tayari watu wawili wameuwawa katika mji wa Suez huku zaidi ya watu 30 wakijeruhiwa vibaya.

Mkuu wa baraza la kijeshi la Misri, Mohamed Hussein Tantawi

Mkuu wa baraza la kijeshi la Misri, Mohamed Hussein Tantawi

Hata hivyo afisa mmoja katika wizara ya afya Mohammed Lasheen amesema wawili hao waliuwawa kwa kupigwa risasi mapema leo asubuhi na kupelekwa katika hospitali moja huko Suez, huku takriban watu 3000 wakiandamana hadi katika makao makuu ya polisi mjini humo. Walioshudia wanasema polisi waliwarushia waandamanaji vitoa machozi na kuwafyatulia risasi. waandamanaji wanalaumu polisi kwa kushindwa kudhibiti ghasia.

Jana zaidi ya watu 600 walijeruhiwa baada ya makabiliano makali na polisi walipojaribu kuivamia wizara ya ndani nchini humo, wanayoilaumu kwa kuhusika na mauaji yaliotokea katika uwanja wa kandanda mjini Port Said.

Raia wa Misri mara kwa mara wamekuwa wakilishutumu baraza la kijeshi linalowatawala kwa kushindwa kushughulikia mambo muhimu nchini humo na pia kushindwa kutekeleza haki za kibinaadam zinazoendelea kukiukwa nchini humo.

Kwa miezi kadhaa sasa waandamanaji wamekuwa wakiandamana wakitaka utawala wa jeshi pamoja na mkuu wa jeshi hilo Hussein Tantawi aliyekuwa waziri wa ulinzi wa rais wa zamani Hosni Mubarak Kuondoka na kukabidhi utawala kwa raia.

Mapigano ya hivi karibuni kati ya mashabiki wa kandanda wa timu hasimu nchini humo yanasemekana kuwa mabaya zaidi kuwahi kutokea katika historia ya kandanda. Wafuasi wa timu ya Al-Masry walimiminika uwanjani baada ya timu yao kuchukua ushindi wa mabao matatu kwa moja dhidi ya timu ya Al-Ahly, na kuanza kuwarushia mawe na chupa na kuanzisha vurugu hilo.

Mwandishi: Amina Abubakar/AFPE
Mhariri: Yusuf Saumu