1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wamisri waendelea kupiga kura

Admin.WagnerD24 Mei 2012

Wamisri wameendelea kupiga kura siku ya Alhamis ambayo ni ya mwisho katika uchaguzi wa kwanza wa rais, tangu kuhitimishwa utawala wa miongo mitatu wa rais Hosni Mubarak kwa nguvu ya umma mwanzoni mwa mwaka jana.

https://p.dw.com/p/151Ub
Uchaguzi Misri.
Uchaguzi Misri.Picha: picture-alliance/dpa

Katika miji ya Cairo na Giza kuliripotiwa kuwepo na uhudhuriaji mdogo wa wapiga kura nyakati za asubuhi, lakini waangalizi walisema zoezi hili lingezidi kuchangamka kadiri muda unavyosonga mbele, hususani nyakati za jioni.

Televisheni ya serikali ilionyesha wapiga kura wakipanga foreni nje ya vituo vya kupigia kura katika maeneno kadhaa nje ya Mji Mkuu Cairo. Wafanyakazi wa serikali nao walipewa siku ya mapumziko kuwawezesha kupiga kura baada ya raia wengi kufurika katika vituo vya kupigia kura siku ya Jumatano.

Wanaotarajiwa kufanya vizuri
Wagombea 13 wanachuana kwa ajili ya kiti hiki cha urais kilichokaliwa na Hosni Mubarak kwa zaidi ya miaka 30 lakini wanaotizamiwa kufanya vizuri ni pamoja mgombea wa chama cha udugu wa kiislam Mohammed Mursi, mwanachama wa zamani wa chama hicho Abdul-Moneim Abul Futouh, Waziri wa zamani wa mambo ya nje katika utawala wa Hosni Mubarak, Amr Moussa, Waziri Mkuu wa mwisho wa Mubarak Ahmad Shafiq na Hamdeen Sabbah anayesimama kwa sera za mrengo wa kushoto.

Wanawake wa Misri wakipiga kura katika kituo kimoja mjini Cairo.
Wanawake wa Misri wakipiga kura katika kituo kimoja mjini Cairo.Picha: Reuters

Zaidi ya raia milioni 50 wana vigezo vya kupiga kura katika taifa hilo lenye watu takribani milioni 80. Wagombea wawili wanatarajiwa kuingia katika duru ya pili itakayofanyika mwezi Juni kama hakutakuwa na mshindi wa moja kwa moja. Watafuta maoni wanasema kuwepo kwa idadi kubwa ya watu ambao hawajaamua nani wa kumchagua kunafanya matokeo ya duru ya kwanza kuwa magumu kutabirika.

Kwa mara ya kwanza, wadadisi wanasema ushindi uko wazi kwa yeyote kati ya wagombea wanaopewa nafasi kubwa katika uchaguzi huu baada ya miongo kadhaa ya kujulikana kwa mshindi hata kabla ya kuanza kwa kampeni.

Changamoto kwa rais mpya
Rais ajaye wa Misri anakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwa ni pamoja na uchumi uliyoyumba kwa kiwango kikubwa tangu kuanza kwa harakati za kumung'oa Hosni Mubarak, kudorora kwa hali ya usalama na kuunganisha raia wa nchi hii waliyogawanywa na mapinduzi na machafuko yaliyojitokeza baadae. Lakini madaraka yake pia bado kubainishwa wazi maana Zoezi la kuandika katiba mpya halijakamilika.

Watafuta maoni wanasema wengi wa wapiga kura ambao hawajaamua nani wa kumchagua lakini watapiga kura wanaweza kufanya maamuzi katika dakika za mwisho au kumchagua mgombea mwenye mtandao mzuri wa uraghibishi.

Raia wa Misri akitekeleza haki yake ya kikatiba.
Raia wa Misri akitekeleza haki yake ya kikatiba.Picha: Reuters

Wanaharakati wa Kiislam ambao walikandamizwa sana wakati wa utawala wa Hosni Mubarak wanataka kujizatiti baada ya kushinda viti vingi katika uchaguzi wa wabunge na sasa wanasema wataweza kutekelza sera zao vizuri kama watapata fursa ya kuunda serikali. Lakini jambo hili linawastua baadhi ya watu wanaohofu kuwa chama cha Udugu wa Kiislam kitaanzisha mfumo wa sheria za kiislam na hivyo kuwabana.

Vituo zaidi ya 13,000 vya kupigia kura vilivyoko katika majimbo 27 nchini Misri vinatarajiwa kufungwa majira ya saa mbili usiku na matokeo rasmi yanatarajiwa kutolewa wiki ijayo.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga\DPAE\APE\AFPE
Mhariri: Mohammed Abdul Rahman.