Waliogombea uchaguzi wa rais Belarus, wakamatwa | Matukio ya Kisiasa | DW | 20.12.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Waliogombea uchaguzi wa rais Belarus, wakamatwa

Wagombea hao ni waliokuwa wanashidana na Rais Alexander Lukashenko wa Belarus katika uchaguzi uliofanyika jana.

default

Rais wa Belarus, Alexander Lukashenko.

Wagombea wanne kati ya tisa ambao walishiriki katika uchaguzi mkuu wa rais uliofanyika jana nchini Belarus dhidi ya Rais Alexander Lukashenko wamekamatwa na polisi hii leo. Taarifa hiyo ni kwa mujibu wa wasaidizi wa wanasiasa hao.

Miongoni mwa waliokamatwa ni Vladmir Neklyayev, ambaye alichukuliwa na polisi kutoka hospitalini alikokuwa amelazwa, muda mfupi baada ya kupigwa na polisi. Wengine ni Andrei Sannikov, mkuu wa kundi la wanaotetea haki, grigory Kostusev, mkuu wa chama cha Nationalist na Nikolai Statkevich, kanali mstaafu wa jeshi, ambaye anakiongoza chama cha Social-Democrat.

Afisa katika ofisi ya mwendesha mashtaka mkuu wa Belarus, Pavel Rodionov amekiambia kituo cha televisheni ya taifa kuwa baadhi ya wagombea hao watafunguliwa mashtaka ya kuandaa maandamano makubwa na huenda wakakabiliwa na kifungo cha hadi miaka 15 jela.

Aidha, msemaji wa Polisi, Konstantin Shalkevich ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa watu wengine kadhaa wamekamatwa jana usiku baada ya polisi wa kutuliza ghasia kuvamia uwanja wa uhuru wa Minsk na kuvunja kundi la maelfu ya waandamanaji wanaompinga Rais Lukashenko.

Upande wa upinzani umedai kuwa wafuasi wa Rais Lukashenko wamefanya udanganyifu katika uchaguzi huo. Mapema leo, Tume ya taifa ya uchaguzi ilimtangaza Lukashenko kuwa mshindi wa uchaguzi huo baada ya kupata asilimia 79.7 ya kura baada ya kura zote kuhesabiwa. Takwimu zilizotolewa na Tume ya uchaguzi zimeonyesha kuwa idadi ya watu waliojitokeza kupiga kura ilikuwa asilimia 90.4. Akizungumzia kuhusu uchaguzi huo, mmoja wa wapiga kura alisema:

Lukashenko ambaye anaunga mkono serikali inayofuata mfumo wa Kisovieti, alizuia maandamano ya watu wengi kabla ya uchaguzi huo na alitishia kutumia nguvu dhidi ya upinzani iwapo watampuuza. Hata hivyo, waandamanaji walijaribu kuingia katika ofisi za Tume ya uchaguzi pamoja na majengo mengine ya serikali na kuvunja vioo na milango. Mwenyekiti wa Tume ya uchaguzi, Lidia Eromoshina amekiita kitendo hicho kuwa ni cha kutisha.

Wakati huo huo, Marekani na Umoja wa Ulaya wamelaani kitendo cha kukamatwa kwa wafuasi wa upinzani. Marekani leo imeishutumu Belarus kwa kutumia nguvu ya ziada dhidi ya waandamanaji hao waliokuwa wakipinga ushindi wa Rais Lukashenko. Taarifa iliyotolewa na Ubalozi wa Marekani mjini Minsk, imeeleza kuwa nchi hiyo inaalani vikali ghasia zilizotokea kutokana na uchaguzi wa jana.

Taarifa hiyo ya Ubalozi wa Marekani imefafanua kuwa serikali ya Belarus imetumia nguvu dhidi ya wafuasi wa upinzani ikiwemo kuwapiga na kuwakamata wagombea hao wa urais pamoja na kudhibiti shughuli za waandishi habari na wanaharakati wa Jumuiya za kiraia.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (RTRE,DPAE,AFPE)

Mhariri:Abdul-Rahman,Mohammed

 • Tarehe 20.12.2010
 • Mwandishi Kabogo Grace Patricia
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/QgHE
 • Tarehe 20.12.2010
 • Mwandishi Kabogo Grace Patricia
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/QgHE

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com