Walibya waendelea kusubiri matokeo ya uchaguzi | Matukio ya Kisiasa | DW | 09.07.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Walibya waendelea kusubiri matokeo ya uchaguzi

Kamati ya uchaguzi ya Libya imesema, matokeo ya awali ya uchaguzi mkuu yanatarajiwa kutangazwa leo jioni au kesho. Waangalizi wa kimataifa wanaeleza kuwa mchakato wa kuhesabu kura unaweza kuchukua siku nne au tano zaidi.

Uchaguzi Libya

Uchaguzi Libya

Uchaguzi uliofanyika wiki iliyopita nchini Libya ni wa kwanza huru kufanyika nchini humo katika muda wa miongo kadhaa. Mwasisi na mtu aliyepanga njama za uasi ambao uliuangusha utawala  wa Moammar Gaddafi, ametoa wito wa kuwa na mazungumzo ya umoja wa  kitaifa. Mahmud Jibril anayeongoza  chama cha  National Forces Alliances, ambacho kinasemekana kuwa kinaongoza kwa mujibu wa  matokeo ya awali na yasiyo rasmi, ametoa wito  kwa vyama vyote kuwa na umoja. Kiongozi  huyo ametaka kufanyika majadiliano  ya  kitaifa, ili kufikiwa kwa muafaka, ambapo muswada  wa  katiba  unaweza  kuandikwa   na  serikali mpya  inaweza kuundwa.

Matamshi  yake  yamekuja muda  mfupi  baada  ya  kiongozi  wa  chama  cha Justice and Construction kukiri kuwa chama cha NFA kinaongoza   katika uchaguzi  huo  katika  mji  mkuu   wa Libya, Tripoli,  pamoja  na  mji  wa  pili kwa  ukubwa   wa Benghazi. Chama  hicho  kimepata  matokeo  mazuri  katika miji  mikubwa  isipokuwa Misrata.

Akizungumza katika mkutano na wandishi wa habari uliofanyika hapo jana usiku, Jibril alisema "Hakuna mshindi wala aliyeshindwa katika uchaguzi uliofanyika. Kwa yeyote atakayeshinda, Libya ndiyo itakuwa imeshinda."

Waangalizi wa kimataifa waridhishwa na uchaguzi

Alexander Graf Lambsdorff wa Umoja wa Ulaya

Alexander Graf Lambsdorff wa Umoja wa Ulaya

Akiuzungumzia uchaguzi wa Jumamosi, mkuu wa kundi la waangalizi kutoka Umoja wa Ulaya, Alexander Graf Lambsdorff, ameusifu kuwa hatua nzuri: "Uchaguzi huu ni mwanzo wa mchakato wa kidemokrasia. Ni lazima tuseme kwamba umekwenda vizuri kuliko tulivyotarajia. Uchaguzi huu umeweka msingi wa maendeleo ya kidemokrasia katika nchi hii. Lakini bado ipo kazi kubwa ya kufanya kwani nchi hii bado haina katiba." Lambsdorffaliongezea kuwa bado yapo maswali muhimu yanayohitaji majibu kama vile suala la kugawana mamlaka au kugawana mapato yatokanayo na uuzaji wa mafuta.

Uchaguzi wa Libya kwa sehemu kubwa ulikuwa shwari. Palikuwa na taarifa za hujuma katika baadhi ya vituo vya kupigia kura vilivyopo mashariki mwa nchi hiyo. Mtu mmoja aliuwawa katika mji wa Ajdabiya baada ya watu waliokuwa wamebeba silaha kukishambulia kituo kimoja cha kupigia kura kwa risasi. Lakini mbali na matukio hayo, zoezi la kupiga kura lilikwenda vizuri na watu wengi waliiona siku ya kupiga kura kama sikukuu.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon, kupitia msemaji wake amewapongeza Walibya kwa kupiga kura na kueleza kwamba zoezi zima lilikuwa limeandaliwa vizuri na kuendeshwa kwa uwazi. Ban amewataka Walibya sasa wakae pamoja na kutunga katiba mpya ya haki na itakayoleta maridhiano huku ikiyajumuisha makundi yote katuka jamii

Mwandishi: Elizabeth Shoo/AFP

Mhariri: Mohammed Khelef

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com