1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakurdi wa Afrin waomba msaada kijeshi wa Syria

Isaac Gamba
26 Januari 2018

Wapiganaji wa Kikurdi katika mji wa Afrin nchini Syria wameomba  msaada wa kijeshi kutoka kwa serikali ya Syria mnamo wakati mashambulizi ya vikosi vya Uturuki dhidi ya wapiganaji hao yakizidi kushika kasi.

https://p.dw.com/p/2rXyZ
Türkei Hatay - Türkische Panzer an der Syrischen Grenze "Operation Olive Branch"
Picha: picture-alliance/AA/F. Aktas

Maafisa  wa Kikurdi  katika mkoa wa Afrin katika taarifa yao wametoa mwito kwa serikali ya Syria  kutekeleza wajibu wao wa kulinda mipaka ya nchi hiyo dhidi ya mashambulizi yanayofanywa na vikosi vya Uturuki.

Mwenyekiti mwenza wa baraza la mji wa Afrin  Othiman Al -Sheikh Issa  alilieleza shirika la habari la AFP kuwa  Rais wa Syria Bashar al-Assad anapaswa kuingilia kati hali hii na kutoruhusu ndege za Uturuki kuruka katika anga ya Syria.

Alisema wana amini kuwa Afrin  ni sehemu ya Syria  na kuwa shambulizi lolote dhidi ya Afrin  ni shambulizi kwa watu  wa Syria pamoja na uchokozi dhidi ya taifa hilo.

Operesheni hii ya  Uturuki katika jimbo la Afrin inaonekana kuwa changamoto kubwa kwa wakurdi katika juhudi zao za  muda mrefu za kutaka kuwa na taifa lao likijumuisha wakurdi walioko  Uturuki na Kaskazini mwa Syria. 

Uturuki ilianzisha mashambulizi mpakani mwa Syria Jumamosi iliyopita dhidi ya wapiganaji wa Kikurdi wenye mafungamano na kundi la YPG ambalo Uturuki inalichukulia kama kundi la kigaidi.

Haya yanajiri mnamo wakati  Uturuki  kupitia kwa msemaji wa  rais Recep Tayyip Erdogan ikitoa mwito kwa Marekani kusitisha uungaji wake mkono kwa wapiganaji wa wakikurdi wa YPG vinginevyo iwe tayari kukabiliana na vikosi vya Uturuki katika mapiagano ya ardhini nchini Syria.

 

Schweiz Davos Weltwirtschaftsforum Donald Trump
Rais wa Marekani Donald TrumpPicha: Getty Images/AFP/N. Kamm

Marekani yasema inafuatilia silaha zinazotumiwa na YPG

Nayo wizara ya ulinzi ya Marekani imesema inafuatilia  kwa makini silaha zinazotumiwa na YPG ili zisije kuangukia katika mikono isiyo salama  na kuwa Marekani   itaendelea pia  na mashauriano na Uturuki.

Marekani imekuwa ikiwaunga mkono wapiganaji wa Kikurdi wa YPG kaskazini mwa Syria  katika mapambano dhidi ya kundi la itikadi kali linalojiita Dola la Kiisilamu hatua ambayo imekuwa haiifurahishi Uturuki.

Tofauti na Marekani, Uturuki inasisitiza kuwa YPG wanamafungamano na chama cha wafanyakazi kilichopigwa marufuku cha PKK.

Waziri  wa Uturuki anayehusika na masuala ya ulaya Omer  Celik amelieleza shirika la habari la AFP kuwa operesheni hiyo kaskazini mwa Syria inalenga  kulinda masilahi ya kiusalama ya Uturuki na pia kulinda usalama wa ulaya.

 Akizungumza hapo jana Alhamisi mjini Brusssels waziri huyo alisema tayari walikwishawaeleza  bayana marafiki na washirika wao juu ya haja ya kutowaunga mkono wapiganaji wa YPG na kuwa wanapaswa kushirikiana katika operesheni hiyo  lakini badala yake hawakufanya hivyo na ndio sababu Uturuki ikaamua  kuanzisha mashambulizi.

Türkei Erdogan Rede Operation Olivenzweig
Rais wa Uturuki Recep Tayyip ErdoganPicha: picture-alliance/AP/M. Cetinmuhurdar

Ingawa rais wa Syria Bashar  Assad  anaonekana kuwa mmoja wa wapinzani wakuu wa Uturuki katika ukanda huo bado kuna mashaka iwapo kiongozi huyo ataitikia wito wa maafisa wa Kikurdi.

Rais Assad mara kadhaa amekuwa akipinga wazo la wakurdi kutaka kuwa na taifa lao na katika siku zilizopita amewahi kutishia kuwasambaratisha wale anaowaita wasaliti wa Syria.

Uturuki pia inasisitiza kuwa ilifikia makubaliano na Urusi ambayo ni mshirika mkuu wa rais Bashar Assad kabla ya kuanzisha mashambulizi hayo nchini Syria.

Mwandishi: Isaac Gamba/dw/afpe

Mhariri: Caro Robi