1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakristo wa Nigeria waapa kujilinda wenyewe

Josephat Nyiro Charo29 Desemba 2011

Baada ya mashambulizi ya bomu dhidi ya madrasa kusini mwa Nigeria, shaka imenza kuzuka kwa kiapo cha Wakristo nchini humo kujilinda wenyewe kufuatia mfululizo wa mashambulizi dhidi yao yaliyofanywa na Boko Haram.

https://p.dw.com/p/13bGk
Sehemu ya mtaa wa Madalla baada ya mashambulizi kwenye sikukuu ya Krismasi.
Sehemu ya mtaa wa Madalla baada ya mashambulizi kwenye sikukuu ya Krismasi.Picha: dapd

Mkuu wa muungano wa Wakristo nchini Nigeria, Mchungaji Ayo Oritsejafor, amewahimiza waumini wasilipize kisasi, lakini akasema wanapaswa kujilinda wenyewe pamoja na mali zao na maeneo ya ibada kwa njia yoyote ile wanayoweza.

"Muafaka ni kwamba jamii ya Wakristo nchi nzima hawatakuwa na chaguo lengine ila kuchukua hatua zifaazo iwapo kutafanywa mashambulio mengine dhidi ya waumini wenzao, makanisa na mali." Amesema mchungaji huyo.

Mchungaji Oritsejafor alikuwa akizungumza akiwa Madalla, karibu na mji mkuu Abuja wakati alipolitembelea kanisa Katoliki la Mtakatifu Theresa, ambako mashambulizi mabaya kabisa yalifanywa, ambapo watu 35 kati ya 40 waliouwawa kwenye msururu wa mashambulizi ya mabomu sikukuu ya Krismasi Jumapili iliyopita, walikufa hapo.

Viongozi wa Kikristo wameihimiza serikali na idara ya ujasusi zichukue hatua zaidi dhidi ya machafuko yanayozidi kufanywa na kundi la Boko Haram. Mchugaji Ayo Oritsejafor ameyaeleza mashambulio hayo kuwa tangazo la vita dhidi ya Wakristo na Nigeria nzima kama taifa.

Hapo jana pia muungano wa makanisa ya Kipentekoste nchini Nigeria ulisema waumini wake watajilinda iwapo mashambulio dhidi yao yataendelea mwaka ujao 2012 na kama maafisa wa serikali watashindwa kuwalinda wakristo. Hata hivyo afisa wa muungano huo alisisita kwamba hawawachochei waumini wajihami na silaha na kuingia kwenye mapigano.

Majeruhi wakitibiwa baada ya mashambulizi ya mabomu dhidi ya kanisa nchini Nigeria.
Majeruhi wakitibiwa baada ya mashambulizi ya mabomu dhidi ya kanisa nchini Nigeria.Picha: dapd

Huku hali ya kukatisha tamaa ikiongezeka kutokana na serikali kutoweza kuyazuia mashambulio licha ya operesheni za kijeshi, rais wa Nigeria, Goodluck Jonathan amesema wanafanya kila wawezalo wakisaidiwa na mataifa mengine barani Afrika na kwingineko yaliyowahi kukabiliwa na mashambulio ya makundi yenye misimamo mikali ya kidini. Rais Jonathan amewataka Wanigeria wasiwafiche wala kuwahifadhi wahalifu.

Maafisa wa serikali wako mbioni kuwapa misaada watu takriban 9,000 waliolazimika kuyakimbia makazi yao katika mji wa Damaturu kaskazini mashariki mwa Nigeria, kufuatia mapambano makali kati ya maafisa wa usalama na kundi la Boko Haram wiki iliyopita. Duru za polisi na za kundi la kutetea haki za binadamu zinasema hadi watu 100 wanahofiwa mjini humo.

Viongozi wa Nigeria wako mbioni kutuliza hali ya wasiwasi huku kukiwa na hofu kwamba huenda yakazuka mapigano kati ya makundi mbalimbali ya kidini nchini humo.

Mwandishi: Josephat Charo/AFPE
Mhariri: Hamidou Oummilkheir