1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakimbizi wa Somalia warejea nyumbani

11 Julai 2013

Maelfu ya wakimbizi wa Somalia wamerejea nchini mwao baada ya hali ya usalama kuimarika katika nchi hiyo. Wengi wa wakimbizi hao walikuwa wanaishi katika kambi iliyoko kaskazini mwa nchi jirani ya Kenya.

https://p.dw.com/p/1967k
Wakimbizi wa Somalia kwenye kambi ya Dadaab, Kenya
Wakimbizi wa Somalia kwenye kambi ya Dadaab, KenyaPicha: Getty Images

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi la UNHCR, limesema kuwa kiasi wakimbizi 20,000 wa Somalia, wamerejea nchini mwao kwa mwaka huu, ingawa huenda wengine wakawa wamerejea kwa muda. Hata hivyo, Umoja wa Mataifa, umesema uko tayari kuwasaidia wakimbizi 60,000 zaidi, ambao wako tayari kurejea nchini Somalia.

Shirika hilo la UNHCR, tayari limewasaidia zaidi ya wakimbizi 16,000 walioko ndani ya Somalia. Mkuu wa shirika hilo, Antonio Guterres amesema kuwa huo ni muda wa matumaini kwa Somalia. Amesema maelfu ya wakimbizi wamerejea nyumbani na kwamba hawawezi kulipuuzia suala hilo na kwamba linahitaji msaada mkubwa kutoka kwenye Umoja wa Mataifa.

Mkuu wa UNHCR, Antonio Guterres
Mkuu wa UNHCR, Antonio GuterresPicha: Reuters

UNHCR yazungumza na serikali ya Kenya

Katika mkutano wake wa jana Jumatano na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Kenya, Joseph Ole Lenku, Guterres amependekeza kuwepo mpango wa kudumu wa kuwarudisha wakimbizi hao makwao. Amesema shirika hilo limeanzisha mpango wa majaribio wa kuwasaidia wakimbizi 60,000 kurejea katika maeneo salama.

Mwezi Disemba mwaka uliopita, serikali ya Kenya ilitangaza mpango wa kuwarejesha kwa nguvu wakimbizi 100,000 wanaoishi kwenye kambi zilizoko maeneo ya mijini. Hatua hiyo ilikosolewa hadi kufikia hatua ya suala hilo kupelekwa mahakamani, na mahakama iliuzuia mpango huo.

Serikali ya Kenya inaandaa mkutano wa kimataifa mwezi ujao wa Agosti kwa lengo la kulijadili suala la kuwarejesha nyumbani wakimbizi wa Somalia. Kambi ya Dadaab nchini Kenya, ndio kambi kubwa ya wakimbizi duniani na inawahudumia wakimbizi 430,000. Idadi hiyo imepungua kutoka 540,000 mwaka 2011, wakati ambapo wimbi la wakimbizi wa Somalia walikimbia kutokana na njaa.

Somalia ina wakimbizi milioni 1.1

Somalia ina jumla ya wakimbizi milioni 1.1, ikiwa ni nchi ya tatu kuwa na wakimbizi wengi duniani, baada ya Afghanistan na Syria. Nusu ya wakimbizi hao wa Somalia, wanaishi kwenye kambi za nchi jirani ya Kenya.

Kenya ina shauku kubwa ya kuwarejesha wakimbizi hao kwa sababu inaamini kwamba wanamgambo wamekuwa wakizitumia kambi za wakimbizi kufanya mashambulizi tangu nchi hiyo ilipopeleka wanajeshi wake nchini Somalia mwaka 2011, kwa lengo la kuwaondoa waasi wa Al-Shabaab wenye mafungamano na mtandao wa kigaidi wa Al-Qaeda.

Mpiganaji wa Al-Shabaab nchini Somalia
Mpiganaji wa Al-Shabaab nchini SomaliaPicha: AP

Hata hivyo, taarifa ya UNHCR imeeleza kuwa hali ya usalama bado haijatulia kwenye maeneo yote ya Somalia, hivyo bado sio sawa kuharakisha kuwarejesha nyumbani wakimbizi hao na kwamba katika eneo la Jubaland ambako vikosi vya jeshi la Kenya vinapambana na Al-Shabaab, hali bado ni tete na mashirika ya kibinaadamu hajawezi kupeleka misaada kwenye eneo hilo.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/RTRE
Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman