1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakenya watamba katika Olimpik

19 Agosti 2008

Kenya yaongoza Afrika katika orodha ya medali wakiwa na medali 7 (2 za dhahabu).

https://p.dw.com/p/F0lG
Franz-Josef Jung, waziri wa ulinzi wa Ujerumani Beijing.Picha: picture-alliance/ dpa

Wakenya wameamka leo wakishangiria ushindi wao wa medali 2 za dhahabu-moja kutoka kwa chipukizi Pamela Jelimo katika mita 800 wanawake na nyengine kutoka kwa Brimin kipruto katika mbio ambazo Kenya inadai ni mali yake-mita 3000 kuruka viunzi. sasa Kenya yatumai kutoroka kesho na taji la mita 1.500 baada ya muamerika mzaliwa wa kenya bernard lagat kuteleza kabla finali.

Leo wanariadha wa mbio za kasi wa Marekani watajaribu kulipiza kisasi kwa wajamaica katika mbio za mita 110 kuruka viunzi.Katika nusu-finali ya dimba la olimpik mahasimu 2 wa Amerika kusini-Brazil na Argentina wanapambana wakati mabingwa wa Olimpik Nigeria wana miadi leo na Ubelgiji.

Baada ya ushindi wao wa jana wa medali za dhahabu na fedha katika mita 800 na dhahabu na shaba katika mita 3000 kuruka viunzi,wakenya sasa wanapania sasa kutoroka hadi Nairobi na medali nyengine ya dhahabu kutoka mita 1500.Mkenya Asbel Kiprop au Augustine Choge watapeana changamoto kali kesho kuania medali hiyo ya dhahabu ambayo katika ubingwa wa dunia mwaka jana huko Osaka,Japan ilikwenda kwa muamerika mzaliwa wa kenya-Bernerd Lagat.

Hali ilikuaje leo mjini Nairobi kufuatia ushindi wa jana ?

Wakenya leo wameamka kwa furaha wakishangiria ushindi wa Brimin kipruto na ule wa chipukizi wao wa miaka 18 Pamela Jelimo katika mita 3000 kuruka viunzi na mita 800 wanawake kwenye uwanja mkuu wa olimpik wa Beijing.

Taarifa za medali hizo 2 za dhahabu pamoja na ile ya fedha ya bingwa wa dunia Janeth Jepkosgei katika mita 800 na medali nyengine ya shaba katika mita 3000 kuruka viunzi ya Richard Mateelong zilichapishwa katika ukurasa wa mbele wa kila gazeti la kenya hii leo.

Gazeti la Daily Nation lilichukua kichwa hiki cha maneno : "SIKU YA KENYA YA DHAHABU NA FAHARI".

Gazeti la STNADARD lilimtangaza chipukizi Jelimo-mkenya wa kwanza kunyakua medali ya dhahabu katika michezo hii ya Beijing "alizaa yayi la dhahabu katika Uwanja wa kyota cha ndege" wa Beijing.

Wakati wa finali hizo 2 alaasiri ya jana, sehemu kubwa ya Kenya ililemaa huku mashabiki wakijikusanya mbele ya rundinga za maafisini au madukani kuwaangalia mashujaa wao wakitamba.

Waziri mkuu Raila Odinga aliwapongeza wakenya hao kwa ushindi wao.

Kilichowafurahisha wakenya zaidi ushindi wa jana wa medali 2 za dhahabu.1 ya fedha na 1 ya shaba umewanyanyua hadi nafasi ya 18 ya orodha ya medali na hata kuipiku Ethiopia.Kenya inaongoza hivi sasa nchi za kiafrika kama taifa kuu la riadha:

Leo Marekani itajiwinda kulipiza kisasi cha kulazwa katika mbio zake za masafa mafupi ya mita 100 na wajamaica tangu wanaume hata na wanawake.Changamoto ya leo ya mbio za mita 100 kuruka viunzi ndipo wamarekani wanakusudia kutoa jibu lao kwani walinyakua nafasi zote 3 za kwanza katika nusu-finali.Mkuki wao unaoongozwa na wasichana bingwa nambari 1 na nambari 2 duniani lolo Jones na Damu Cherry.

Hata bingwa wa rekodi ya dunia ya mita 100 wanaume na bingwa wa olimpik Usain bolt anarudi uwanjani katika nusu-finali ya mita 200 .Bolt analenga mataji yote 2 kuyapeleka Kingston,Jamaica-mita 100 na 200.hii itakua mara ya kwanza tangu Carl Lewis kufanya hivyo katika michezo ya Olimpik ya Los Angeles,1984.

Nje ya medani ya riadha-athletics-dimba linarudi uwanjani leo upande wa wanaume baada ya jana timu ya wasichana ya Brazil kuilipizia kisasi ile ya wanawake ya Ujerumani mabingwa wa dunia kwa kuichapa mabao 4:1.

Hivi ndivyo mchezaji mmoja wa mabingwa wa dunia ujerumani alivyolalamika baada ya mpambano wa jana na Brazil:

"Hatukucheza barabara nyuma-ndio sote tulikusudia kucheza uzuri,lakini tumefanya makosa mengi katika ulinzi na timu kama Brazil haichi kutumia makosa hayo kutamba."

Upande wa timu za wsanaume leo ni leo na asemae kesho mwongo:

mahasimu 2 wa dimba wa Amerika kusini-Brazil na Argentina wanapambana katika nusu finali 2 za leo kuania nafasi ya finali:

Ni changamoto kati ya ronaldinho na Lionel Messi.

Brazil leo imepania kulipiza kisasi kwa kulazwa na Aregentina katika finali ya olimpik ya Athens, 2004.Pia haikuwahi kutawazwa mabingwa wa olimpik na mara hii wanataka kuvunja mwiko huo.

Katika nusu-finali ya pili leo mabingwa wa olimpik 1996 huko Atlanta,Nigeria wana miadi na Ubelgiji kunyakua tiketi ya finali ama na Aregntina au Brazil.