1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waititu atimuliwa kama Gavana wa jimbo la Kiambu, Kenya

Amina Mjahid
30 Januari 2020

Bunge la Seneti nchini Kenya limeidhinisha kutimuliwa kwa Gavana wa jimbo la Kiambu Ferdinand Waititu, baada ya kukutwa na makosa matatu ya matumizi mabaya ya mamlaka, ukiukaji wa katiba na ulaji rushwa.

https://p.dw.com/p/3X32U
Ferdinand Waitutu
Picha: DW/S. Wasilwa

Spika wa bunge la Seneti Ken Lusaka alitoa uamuzi huo wa kumtimua Gavana waititu baada ya mjadala mkali uliofanyika kwa siku mbili mfululizo.

Hata hivyo mgawanyiko ulioko katika chama cha Jubilee ulibainika wakati wa upigaji wa kura pamoja na urafiki mpya kati ya rais Kenyatta na kiongozi wa Upizani Raila Odinga ukiashiria kusambaratika kwa mahusiano kati ya rais na makamu wake William Ruto.

Licha ya kikundi cha maseneta kinachoegemea makamu wa rais William Ruto cha Tangatanga kujaribu kuokoa unga wa gavana huyo wa Kiambu, juhudi zao ziliambulia patupu.

Nacho kikundi cha maseneta kinachoegemea upande wa rais kiliungana na upande wa Upinzani wa NASA na kupiga kura kushikilia makosa matatu ambayo Waititu alikuwa akituhumiwa nayo.

"Hoja yenyewe ina uzito, ukiangalia upande wa matumizi ya kifedha, kuna matatizo. Upande wa kuajiri watu… tufanye linastohili ili wajue seneti inafanya kazi na iwe funzo kwa maseneta wengine,” alisema Issa Juma seneta wa Upinzani.

Baadhi ya viongozi wakuu serikalini wadai Waititu hakutendewa haki

Ferdinand Waititu
Picha: DW/S. Wasilwa

Mwezi Desemba mwaka uliopita, bunge la jimbo la Kiambu lilipiga kura ya kumuondoa afisini gavana Waititu ambaye anakabiliwa na kesi mahakamani baada ya Tume ya Kukabilina na Ufisadi nchini Kenya kukusanya ushahidi wa kufuja fedha za umma.

Wakiongozwa na kiongozi wa wengi katika bunge hilo Kipchumba Murkomen, upande wa Tangatanga ulidai kuwa Waititu hakufanyiwa haki na kwamba mchakato huo ulizongwa na siasa.

Bunge hilo lilimtuhumu, Waititu kwa kutumia fedha zilizotengewa ujenzi wa barabara hivyo kusababishia jimbo hilo hasara kubwa. Aidha alituhumiwa kukiuka sheria ya taifa katika utendaji kazi wake huku akiweka fedha hizo kwenye akaunti ya mwanaye na pia kumnyanganya kipande cha ardhi mama mjane.

Spika wa Bunge hilo Ken Lusaka tayari ameandika uamuzi wa seneti kwenye jarida rasmi la serikali. Makamu wake anatarajiwa kula kiapo na kuanza kazi mara moja. Hii sio mara ya kwanza kwa uamuzi kama huo kuchukuliwa.

Gavana wa Embu Martin Wambora aliokolewa na mahakama baada ya seneti kuunga hoja ya kumbandua afisini.

Chanzo: Shisia Wasilwa, DW, Nairobi