Waisraeli wauawa Bulgaria | Matukio ya Kisiasa | DW | 19.07.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Waisraeli wauawa Bulgaria

Waziri wa mambo ya ndani wa Bulgaria amesema watalii watano wa Israel waliuawa kutokana na shambulio la kujitoa mhanga

Watalii wa Israel waliojeruhiwa wakipelekwa hospitali

Watalii wa Israel waliojeruhiwa wakipelekwa hospitali

Waisrael hao walishambuliwa ndani ya basi katika mji wa Burgas nchini Bulgaria. Katika shambulio hilo dereva wa basi aliekuwa raia wa Bulgaria pia aliangamia.

Waziri wa mambo ya ndani wa Bulgaria Tsevetanov amearifu kwamba mshambuliaji wa kujitoa mhanga aliekuwa amevaa nguo za kujitambulisha kama mtalii alilifanya shambulio hilo,ambapo yenye mwenyewe pia alikufa.

Hata hivyo waziri huyo Tsevetan Tsvetanov amesema nasaba ya mtu huyo bado haijajulikana. Mtu huyo alikuwa amevaa kaptura na alikuwa amebeba mfuko wa mgongoni-shanta na alionekana kama mtalii mwengine yeyote. Hati yake ya kusafiria ilikuwa leseni ya kuendeshea gari kutoka jimbo la Michigan la Marekani. Lakini hati hiyo ilikuwa bandia.

Watu wengine zaidi ya 30, waliokuwamo ndani ya basi pamoja na wapita njia walijeruhiwa.

Hapo awali Israel iliionyeshea kidole Iran.Waziri wa ulinzi wa Israel Ehud Barak amesema Israel inakabailiwa na wimbi la ugaidi linalodhaminiwa na Iran. Waziri Barak amesema shambulio la jana katika mji wa Burgas nchini, Bulgaria lilifanywa na Hezbollah kwa udhamini wa Iran. Waziri huyo wa Israel aliiambia radio ya serikali kuwa mitandao ya Waislamu wenye siasa kali inafanya mashambulio duniani kote na alitoa mifano ya mashambulio ya hivi karibuni, na majaribio ya mashambulio yaliyowalenga Waisraeli.

Hapo jana Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu pia alizinyooshea kidole Iran na Hezbollah kwa kuhusika na mauaji ya watalii nchini Bulgaria. Netanyahu alisema,dalili zote zinaonyesha kuwa Iran ilihusika.

Naye Waziri wa mambo ya nje wa Israel Avigdor Lieberman amesema ni Hezbollah, wakisaidiwa na Iran waliofanya shambulio la kujitoa mhanga.Waziri huyo amedai kuwa taarifa hiyo ni ya kuthibitika na kuongeza kwamba nchi yake inakabiliwa na ugaidi wa kimataifa unaofadhiliwa na kuongozwa na Iran.

Shambulio la jana lililokuwa baya sana, dhidi ya Waisrael, nje ya nchi yao tokea mwaka wa 2004 lilifanyika katika kumbukumbu ya lile lililofanyika nchini Argentina mnamo mwaka wa 1994 ambapo wayahudi 85 waliangamizwa.

Miongoni mwa watu waliojeruhiwa katika shambulio la jana ni vijana ni wenye umri wa kati ya miaka 15 na 19. Mama mmoja mjamzito pia alikuwa miongoni mwa watalii waliojeruhiwa.

Rais Obama ameyaalani mauaji ya mjini Burgas.Amesema shambulio lililosababisha mauaji hayo ni la kinyama. Rais Hollande wa Ufaransa pia ameyaita mauaji hayo kuwa ni ya kinyama. Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Hillary Clinton aliefanya ziara nchini Israel hivi karibuni amesema amehuzunishwa, lakini pia amekasirishwa na mauaji hayo.

Wakati huo huo msemaji wa jeshi la Israel amearifu kwamba ndege ya kwanza inayowarudisha nyumbani watalii wa Israel waliojeruhiwa katika shambulio la mjini Burgas,nchini Bulgaria inatarajiwa kutua Israel jioni.

Mwandishi:Mtullya Abdu/AFPE/RTRE/

Mhariri:Abdul-Rahman

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com