Waisrael na Wapalastina watakiwa wajizuwie
5 Aprili 2018
Katika pande zote mbili za mpaka wa Gaza, watu wanajiandaa kwa wimbi jengine la maandamano makubwa ya Wapalestina yaliyopangwa kuitishwa siku ya Ijumaa, wiki moja baada ya mapambano pamoja na wanajeshi wa Israel kusababisha damu nyingi kabisa kumwagika, tukio ambalo halijawahi kushuhudiwa tangu miaka kadhaa iliyopita. Idadi jumla ya waliouwawa inafikia watu 21 baada ya bwana mmoja kufariki dunia kutokana na majeraha-wizara ya afya ya Gaza imesema. Idadi ya wahanga ilifikia watu 20 baada ya kijana wa miaka 34 kuuliwa kwa mizinga ya ndege za kivita za Israel, alipokuwa anakurubia uzio wa usalama uliowekwa na Israel huko Gaza.
"Vikosi vya usalama vya Israel havitomruhusu yeyote kudhuru usalama wa raia wa Israel na vitaendelea kupambana na magaidi wanaohusika na visa vya kigaidi" jeshi la Israel limesema katika taarifa yake.
Ofisi kuu ya uwiano pamoja na Wapalestina , imewaonya Wapalastina dhidi ya madhara ya kimazingira yanayotokana na kutiwa moto mipira ya magari, huku waziri wa usalama wa jamii Gilad Erdan akisema maandamano yatakuwa na madhara kwa wakaazi wote wa Gaza.
B'Tselem lawataka wanajeshi wa Israel wasitii amri ya kufyetua risasi
Shirikia linalopigania haki za binaadam nchini Israel B'Tselem limewatolea wito wanajeshi wasiwafyetulie risasi waandamanaji kesho ijumaa na ikilazimika, wapuuze amri ya viongozi wao."Ni kinyume na sheria kuwafyetulia risasi waandamanaji wasiokuwa na silaha na amri kama hiyo ni kinyume na sheria, shirika hilo limesema katika taarifa yake.
Maelfu ya Wapalestina waliongozana wakibeba bendera na kupiga kambi karibu na mpaka wiki iliyopita kwa kile walichokiita "Maandamano makubwa ya kurejea nyumbani"-maandamano yatakayodumu wiki sita hadi Mei 15, siku ambayo Israel itaadhimisha miaka 70 tangu ilipoundwa huku Wapalestina nao wakikumbuka siku waliyotolewa katika maskani yao au Al Nakba, neno la kiarabu linalomaanisha "Balaa."
Maandamano makubwa zaidi yahofiwa kutokea kesho katika maeneo ya utawala wa ndani wa Palastina
Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa katika eneo la mashariki ya kati Nickolay Mladenov ameihimiza Israel "ijizuwie na kuwataka Wapalestina waepukane na ugonvi wakati wa maandamano yao katika eneo la mpakani la Gaza. Wito wa Nickolay Mladinov umetolewa katika wakati ambapo hofu zimeenea za kuzuka machafuko makubwa zaidi baada ya sala ya ijumaa. Mladenov amewataka pia wanajeshi wa Israel wajizuwie huku Wapalestina akiwasihi waepukane na ugonvi katika eneo la mpakani. Maandamano na malalamiko lazima yaruhusiwe kuendelea kwa njia ya amani. Raia na hasa watoto wasitiwe hatarini kwa njia yoyote ile, amesisitiza.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/dpa/Reuters
Mhariri: Iddi Ssessanga