1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Siku ya mwisho ya Kampeini Israel

16 Machi 2015

Wagombea katika uchaguzi wa Bunge nchini Israel wako mbioni kuwashawishi wapiga kura katika dakika za mwisho za kampeini kabla ya uchaguzi huo hapo kesho

https://p.dw.com/p/1ErP9
Kiongozi wa mrengo wa Kati kushoto Isaac Herzog
Kiongozi wa mrengo wa Kati kushoto Isaac HerzogPicha: picture-alliance/EPA/JIM HOLLANDER

Leo (16.03.2015) ni siku ya mwisho ya kamepeni ya uchaguzi wa bunge ambao unaangaliwa kama kipimo kitakachoamua juu ya kuendelea kuwepo kwaw waziri mkuu Netanyahu kwa awamu nyingine madarakani.

Matokeo ya kura za maoni za hivi karibuni yameonyesha kwamba chama cha waziri mkuu huyo cha Likud kiko nyuma ya muungano wa kizayuni unaotajwa kuwa na nafasi ya kuongoza kwa kiasi viti vinne mbele ya Likud.

Hata hivyo idadi hiyo ya viti zaidi bungeni kwa chama hicho haina maana kwamba inaweza kumzuia Netanyahu kupata nafasi ya kuunda serikali ijayo,ingawa ni hali iliyokitia wasiwasi mkubwa chama cha Likud kilichoamua hivi sasa kujitokeza kwa nguvu zote kuwashawishi wapiga kura wajitokeze kukichagua chama hicho.

Netanyahu amekuwa akiendeleza juhudi za kuwavutia wapiga kura na kuwashawishi kabla ya uchaguzi wa Jumanne. Hata hivyo mpinzani wake wa chama cha mrengo wa kati Isaac Herzog anatafuta njia za kurekebisha mahusiano na wapalestina pamoja na Jumuiya ya Kimataifa na katika kampeini yake ametoa ahadi ya kuleta nafuu kwa watu wa tabaka la kati nchini Israel.

Benjamin Netanyahu a´kiwa na wabunge wa chama chake Jan 23
Benjamin Netanyahu a´kiwa na wabunge wa chama chake Jan 23Picha: Reuters

Kwa upande wake Netanyahu amekuwa akionekana siku za hivi karibuni katika mahojiano mbali mbali akitahadharisha dhidi ya kuingia kwa serikali ya mrengo wa kushoto.Hata hapo jana alitoa kauli kama hiyo mbele ya maelfu ya wafuasi wa wakihafidhina mjini Tel Aviv.Alisikika akisema kwamba chama cha Likud kiko katika mapambano makali mapambano ambayo inabidi kuibuka na ushindi ili kulifunga pengo lililopo. Netanyahu amekuwa akiwashutumu wapinzani wake wa mrengo wa kati kushoto Issac Herzog na Tzipi Livni kwa kuwa tayari kulitupa mkono wazo la kuifanya Jerusalem kuwa mji mkuu pekee wa Israel katika mazungumzo na wapalestina.

Pamoja na hayo lakini hakuna upande wowote unaotarajiwa kupata zaidi ya robo ya wapiga kura kwahivyo kinachotarajiwa ni kwamba uchaguzi huo huenda ukafuatiwa na kipindi kirefu cha mashauriano kuhusu serikali mpya.

Mtu anayeonekana kuwa na nafasi ya kuamua juu ya nani aunde serikali mpya ni Moshe Kahlon wa chama kipya cha mrengo wa kati na ambaye amekuwa akiendesha kampeini zake chini ya msingi wa suala la uchumi na kuyaweka pembeni kidogo masuala ya changamoto za kidiplomasia zinazoikabili Israe.Kahlon anataka kuwa waziri wa fedha katika serikali ijayo na huenda akaamua kumuunga mkono Netanyahu au Herzog.Kahlon ana asili ya Libya na ni maarufu mbele ya waisraeli wa tabaka la kati kutokana na historia yake katika mashariki ya kati,malezi aliyoyapata pamoja na kufanikiwa kuleta mageuzi katika soko la simu za mkononi nchini humo.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman