1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahariri washtushwa na ripoti ya tume juu ya siasa kali

Abdu Said Mtullya24 Januari 2012

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo wanatoa maoni juu ya ripoti ya tume huru kuhusu chuki dhidi ya wayahudi miongoni mwa wajerumani. Wahariri hao wameshtushwa na ripoti hiyo.

https://p.dw.com/p/13pGK
Tume huru yatoa ripoti juu ya chuki dhidi ya wayahudi nchini Ujerumani.Picha: picture-alliance/dpa

Tume hiyo iliyoundwa na Bunge imesema katika ripoti yake kwamba humusi moja ya wajerumani wana hisia za chuki dhidi ya wayahudi. Katika kila wajerumani watano mmoja ana hisia za chuki dhidi ya wayahudi kifuani.

Juu ya ripoti hiyo, mhariri wa gazeti la Wetzlarer Neue anasema , nchini Ujerumani bado panakosekana mchakato wa kukabiliana na itikadi za kifashisti, zinazowezesha kufanyika mfululizo wa mauaji. Mhariri wa gazeti la Wetzlarer pia anatilia maanani kwamba tume iliyofanya uchunguzi imebainisha kuwa, mgogoro wa Mashariki ya Kati haujashughulikiwa kwa moyo wote na hivyo unawapa wanaitikadi kali wa Kiislamu na nchi kama Iran, mwanya wa kuutumia mgogoro huo ili kuchochea chuki dhidi ya wayahudi. !

Gazeti la Der neue Tag linatoa maoni juu ya uamuzi wa watu wa Croatia wa kujiunga na Umoja wa Ulaya. Mhariri wa gazeti hilo anasema ni wazi kabisa kwamba Croatia na hata Serbia ni sehemu ya Ulaya. Baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe katika neo la kusini mashariki mwa Ulaya, Croatia ni sehemu ya jumuiya ya amani , ambayo sasa inaingia katika mwaka wa 60 wa historia yake.

Lakini mhariri anasema kizingiti kikubwa ni mgogoro wa Euro. Ikiwa hautapatiwa ufumbuzi, hakuna nchi nyingine katika eneo la Balkani itakayoifuata Croatia. Umoja wa Ulaya umepitisha vikwazo zaidi dhidi ya Iran, katika juhudi za kuishinikiza nchi hiyo iachane na mpango wake wa nyuklia. Lakini wahariri wa magazeti wanasema vikwazo vitaleta ufanisi ikiwa nchi zote duniani zitashiriki.

Gazeti la Donakurier linaeleza kwamba kuiwekea Iran vikwazo ni jambo zuri lakini, havitafanikiwa ikiwa wanunuzi wa mafuta ya nchi hiyo hawatasimama pamoja. China, India na hata Uturuki zinavutia kamba upande mwingine.! Gazeti la Donerkurier linasema ikiwa Iran italazamika kulikosa soko la Umoja wa Ulaya kwa ajili ya mafuta yake, hilo halitaishtua nchi hiyo. Itawapata wateja wapya katika bara la Asia na hivyo kuweza kuendelea na mpango wake wa kinyuklia.

Gazeti la Badische Neueste Nachrichten linasema mvutano baina ya nchi za magharibi na Iran unaweza kuondolewa kwa njia za kidiplomasia.Gazeti hilo linasema Ujerumani na Umoja wa Ulaya wakati wote zimekuwa na uhusiano mzuri wa kiuchumi na Iran na kutokana na hali hiyo, zinaweza kuitumia turufu ya kidiplomasia ili kuweka Iran sawa. Lakini gazeti linasikitika kwamba sera za nje za Umoja wa Ulaya hazimo katika mkondo sahihi wa kuutatua mgogoro na Iran.

Mwandishi/Mtullya abdu/Deutsche Zeitungen/

Mhariri/Mohamed Abdul-Rahman