1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani watoa maoni juu ya ziara ya Kansela Merkel barani Afrika

Abdu Said Mtullya11 Julai 2011

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel leo ameanza ziara ya nchi tatu barani Afrika:

https://p.dw.com/p/11syH
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel.Picha: AP

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo wanazungumzia juu ya ziara ya Kansela Merkel barani Afrika inayoanzia nchini Kenya.

Wahariri hao pia wanatoa maoni ya mtamauko kufuatia timu ya kandanda ya Ujerumani kutolewa kwenye kombe la dunia. Na wanazungmzia juu ya umasikini uliopo nchini Ujerumani miongoni mwa baadhi ya wastaafu.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel leo anaanza ziara ya nchi tatu barani Afrika. Ziara hiyo inafanyika muda mfupi tu baada ya Ujerumani kuipitisha sera mpya juu ya Afrika,inayoweka mkazo juu ya ushirikiano,badala ya Ujerumani kutoa misaada tu kwa waafrika!

Mhariri wa gazeti la Neue Osnabrücker anasema ziara hiyo ni ishara sahihi.Mabara ya Afrika na Ulaya yanagusana lakini siyo katika namna inayostahili. Kwa muda mrefu Ulaya imeweka mkazo katika mabara mengine. Kile ambacho Afrika imekuwa inakiambulia kutoka Ulaya, ni makombo au mifuko ya taka, au malori ya silaha, na athari za mabadiliko ya hali ya hewa ambazo hazikusababishwa na nchi za Afrika.

Mhariri huyo anaeleza kuwa Afrika ni bara muhimu kuhusu masuala ya nishati na hali ya hewa. Kwa hiyo bara hilo siyo mwombaji tu.Ni kutokana na hayo kwamba ziara ya Kansela Merkel barani Afrika ni ishara nzuri.

KOMBE LA DUNIA:

Washabiki wa timu ya Ujerumani walitoa pumzi ya mtamauko mwishoni mwa wiki iliyopita, wakati wakiiona timu yao ikiangushwa na akina dada wa Japan na hivyo kutolewa katika mashindano ya kombe la dunia. Ujerumani ilikuwa inalitetea taji la ubingwa. Lakini mambo yalienda mrama na ikalazwa bao moja kwa bila.

Juu ya hayo mhariri wa gazeti la Hannoversche Allgemeine anasikitika lakini wakati huo huo anawashauri washabiki wa timu ya Ujerumani waonyeshe moyo wa kimichezo. Mhariri wa gazeti hilo anaeleza kuwa safari hii michezo haikufuata vigezo vya utabiri. Kwa upande mwigine hilo ni jambo zuri. Mashindano ya kombe la dunia bado yanaendelea ,wakati mwenyeji Ujerumani imetolewa nje. Mhariri wa gazeti la Hannoversche Allgemeine anawaambia washabiki wa kandanda wa Ujerumani kuwa sasa ni fursa kwao kuonyesha moyo wa kimichezo. Lakini pia anasema ni jambo la kusikitisha kwamba timu ya akina dada wa Ujerumani itabakia kwenye mabenchi ya watazamani tu.!


Gazeti la Landeszeitung leo linazungumzia juu ya umasikini uliopo nchini Ujerumani miongoni mwa wazee na hasa wastaafu na linasema, licha ya Ujerumani kuwa injini ya ustawi,watu zaidi na zaidi wanarukwa na neema inayotokana na ustawi huo. Wazee na hasa wastaafu wanachakura chakura katika mapipa ya uchafu kutafuta chupa za kuziuza. Na hali ya wastaafu itakuwa mbaya zaidi kuanzia mwaka wa 2030 ambapo wastaafu watalipwa asilimia 43 ya mishahara yao halisi kama mafao ya uzeeni. Sasa, wakati Ujerumani inapata ustawi mkubwa, ni mahala pa kufikiria juu ya kuweka akiba, badala ya kufikiria juu ya kupunguza kodi.

Mwandishi/Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen/

Mhariri/-Yusuf Saumu