WAHARIRI WA MAGAZETI YA UJERUMANI WATOA MAONI JUU YA UAMUZI WA BUNGE LA SLOVAKIA | Magazetini | DW | 12.10.2011
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Magazetini

WAHARIRI WA MAGAZETI YA UJERUMANI WATOA MAONI JUU YA UAMUZI WA BUNGE LA SLOVAKIA

Wahariri wa magazeti wataka mageuzi katika mfumo wa Umoja wa Sarafu ya Euro.

default

Rais wa Slovakia Ivan Gasparovic.

Bunge la Slovakia limeupinga mpango wa kuongeza fedha katika mfuko wa kuziokolea nchi zenye madeni zilizomo katika Umoja wa sarafu ya Euro. Wahariri wa magazeti wanatoa maoni yao juu ya uamuzi wa Bunge hilo.

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani pia wanatoa maoni yao juu ya hukumu iliyotolewa kwa aliekuwa Waziri Mkuu wa Ukraine, Tymoshenko.

Mhariri wa gazeti la Nürnberger Nachrichten anasema uamuzi wa wabunge wa Slovakia unaonyesha ni kwa kiasi gani mfumo wote wa Euro unavyohitaji kufanyiwa mageuzi. Mhariri huyo anaongeza kwa kusema kuwa nyanja nyingine zote za mfumo wa Ulaya pia zinapaswa kufanyiwa mageuzi.

Mhariri wa Nürnberger Nachrichten anauliza, inakuaje kwamba mustakabali wa jumuiya nzima ya sarafu ya Euro unategemea uamuzi wa Bunge la nchi moja , ambayo , kumradhi, haina uzito wowote? Mhariri huyo anasema njia ya kuuzuia ushawishi mkubwa wa mabenki ni kutekeleza sera ya pamoja.

Mhariri wa gazeti la Neue Osnabrücker pia ametoa maoni yake juu ya uamuzi wa Bunge la Slovakia, lakini kwa kuzitaka nchi kama Ujerumani zijitazame katika kioo kwanza,kabla ya kulalamika juu ya Bunge la Slovakia. Mhariri huyo anaeleza kuwa nchini Ujerumani pia ruzuku kubwa zinatolewa kwa waajiri na waajiriwa kadhalika- kuanzia posho kwa wenye magari, pensheni kubwa kwa watumishi wa serikali na posho za kijamii. Anasema wakati sasa umefika wa kuuangalia mfumo huo nchini Ujerumani vilevile, badala ya kushangaa juu ya uamuzi wa Bunge la Slovakia.

Gazeti la Kölner Stadt Anzeiger linasema kinachohitajika sasa ni hatua za haraka ili kuutatua mgogoro wa madeni. Gazeti hilo linaeleza kwamba siyo tu nchini Slovakia, bali pia nchini Ujerumani, Finland na Ufaransa ,hatua zinazochukuliwa zimeshapitwa na wakati. Hayo yamethibitika baada ya mkutano wa Kansela Merkel na Rais Sarkozy. Viongozi hao wanatayarisha hatua nyingine, kwani maamuzi yaliyopitishwa kwenye mkutano wa kilele wa viongozi wa Umoja wa Ulaya tayari yameachwa nyuma na wakati.

Hapo jana mahakama ya nchini Ukraine ilitoa hukumu ya kifungo cha miaka saba jela kwa aliekuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Julia Tymoshenko. Sababu, ni ati kwamba alitia saini mkataba wa biashara na Urusi ulioitia hasara nchi yake! Gazeti la Donaukurier linatoa maoni yake kwa kusema kwamba hukumu hiyo inakumbusha yaliyomfika mfanya biashara maaruf wa Urusi, Chodorkovsky ambae yumo jela tokea miaka 7 iliyopita. Putin alitaka iwe hivyo alipokuwa Rais nchini Urusi. Na sasa Rais Yanukovych wa Ukraine ametumia njia hiyo hiyo ili kumzima mpinzani wake.

Gazeti la Märkische Allgemeine linamtaka Kansela wa Ujerumani Angela Merkel afikirie upya juu ya dhima ya Ujerumani katika mchakato wa kuongeza fedha katika mfuko wa kuziokolea nchi zenye madeni barani Ulaya!

Mwandishi:Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen/

Mhariri: Othman,Miraji

 • Tarehe 12.10.2011
 • Mwandishi Abdu Said Mtullya
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/12qsB
 • Tarehe 12.10.2011
 • Mwandishi Abdu Said Mtullya
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/12qsB