1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahariri , juu ya ndoa za jinsia moja

Abdu Said Mtullya24 Aprili 2013

Pamoja na masuala mengine wahariri hao leo wanazungumzia juu ya uamuzi wa Bunge la Ufaransa wa kuzipitisha ndoa za jinsia moja.

https://p.dw.com/p/18M6F
Rais wa Ufaransa Francois Hollande
Rais wa Ufaransa Francois HollandePicha: Reuters

Juu ya ndoa za jinsia sawa nchini Ufaransa mhariri wa "Süddeutsche Zeitung "anasema maalfu kwa maalfu ya watu miongoni mwao vijana walionyesha ghadhabu dhidi ya serikali na hali ya kijamii kwa jumla.Gazeti hilo linatilia maanani kwamba watu hao wanadhamiria kuendelea kupinga hata baada ya Bunge la nchi yao kuipitisha sheria ya kuruhusu ndoa za jinsia sawa. Na kwa hakika watu hao hawaipingi tu sheria hiyo ,bali kwa jumla wanazipinga siasa za Rais Hollande. Kwa mtazamo wa watu hao,si wasoshalisti wala wahafidhina wa chama cha UMP, wenye uwezo wa kuwapa watu matumaini na kuwaondolea hofu walizonazo.

Upinzani utaendelea:

Naye mhariri wa gazeti la "Die Welt"anasema upinzani dhidi ya sheria ya kuhalalisha ndoa za jinsi moja utaendelea, lakini juhudi za chama cha upinzani,UMP zimechelewa. Mhariri huyo anaeleza kwamba chama cha upinzani cha UMP kinadhamiria kuenda mbele ya Baraza la katiba ili kuipinga sheria hiyo. Hata hivyo matumaini ya kufanikiwa ni madogo.Kilichobakia ni kusubiri hadi chama hicho kiingie madarakani mnamo mwaka wa 2017,ikiwa kitafanikiwa.Lakini hadi wakati huo ndoa nyingi za jinsia sawa zitakuwa zimeshafungwa nchini Ufaransa na kuwa jambo la kawaida kama ilivyo katika nchi nyingine nane za Ulaya.

Hesabu za Hollande zaenda mrama:

Gazeti la "Badische Neueste Nachrichten" linasema Rais Hollande hakupiga hesabu zake vizuri juu ya suala la ndoa za jinsia moja. Mhariri wa gazeti hilo anaeleza kwamba Rais Hollande amepuuza ukweli kwamba Ufaransa ni jamii yenye taathira kubwa ya uhafidhina wa wakatoliki. Jinsi serikali yake ilivyolishughulikia suala hilo na kutokana na udhaifu wa mawasiliano upinzani ambao hapo awali ulikuwa mdogo umegeuka kuwa wimbi kubwa la upinzani. Hollande ameshinda raundi ya kwanza bungeni lakini pambano bado halijafika raundi ya mwisho.

Silaha kwa waasi wa Syria?
Mhariri wa "Neue Osnabrücker" anauzungumzia mgogoro wa Syria kwa kutilia maanani kwamba wapinzani wanakabiliwa na mikingamo, na hivyo inakuwa vigumu kuwaunga mkono wapinzani hao kwa kuwapa silaha.

Mhariri wa gazeti hilo anaeleza kuwa katika mgogoro wa Syria ni vigumu kupambanua baina ya mema na mabaya.Maaskofu wanatekwa nyara,kuna habari juu ya kutumiwa kwa silaha za nyuklia.Pande za serikali na upinzani zinatupiana lawama. Hali inazidi kuwa ngumu kutokana na wapinzani kuungwa mkono na makundi mbalimbali.Katika hali hiyo ,pendekezo la baadhi ya wanachama wa Umoja wa Ulaya juu ya kuwapa silaha wapinzani ni gumu.

Mwandishi:Mtullya abdu/Deutsche Zeitungen.

Mhariri: Josephat Charo