Wahanga wa vita wakumbukiwa | Magazetini | DW | 20.11.2006
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Wahanga wa vita wakumbukiwa

Suala kuu katika magazeti ya leo ni hotuba aliyoitoa Rais Horst Köhler wa Ujerumani jana, Jumapili, ambapo ilikuwa siku ya kuwakumbusha wahanga wa vita vikuu vya dunia. Köhler pia alikumbusha pia wale wanajeshi waliouawa nchini Afghanistan katika miaka iliyopita.

Wakati huo huo, serikali ya Ujerumani inaendelea kupinga wanajeshi wake kupelekwa katika eneo la Kusini mwa Afghanistan ambako mapigano ni makali zaidi. Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wanaiunga mkono serikali hii.

Katika gazeti la “Handelsblatt” la mjini Düsseldorf tunasoma yafuatayo:
“Ikiwa inataka kuyahatarisha maisha ya wanajeshi wake, lazima serikali ya Ujerumani iangalie hali nzima ya vita na usalama duniani. Huko Mashariki ya Kati, Marekani haipingi kabisa Israel, lakini nchini Irak na Afghanistan, inachukua msimamo mkali wa kijeshi. Kama Ujerumani ingekubali kusaidia kijeshi tu bila ya usemi wowote wa kisiasa, basi ingepotea kabisa ushawishi wake katika siasa za kigeni.”

Mhariri wa gazeti la “Abendzeitung” kutoka Munich aliandika maoni haya:
“Inafahamika kwamba wanajeshi wa ISAF walioko Kusini mwa Afghanistan walikasirika kwamba huko Kaskazini ambapo Wajerumani wanaongoza hatua ya kijeshi, hali ni ya usalama zaidi. Hata hivyo, hakuna haja ya kulikosoa jeshi la Ujerumani, Bundeswehr. Wanajeshi hawa wanatoa mchango mkubwa katika kujengwa upya Afghanistan na kuimarisha biashara wakiungwa mkono na Waafghanistani. Mkakati wa Marekani na Uingereza lakini ni kushambulia kwa mabomu tu.”

Baada ya mapigano kati ya Israel na Palestina kuendelea mwishoni mwa wiki iliyopita, mhariri wa gazeti la “Braunschweiger Zeitung” ametoa maoni yake kuhusu matokeo haya na kuandika:
“Ikiwa kuna mwanasiasa yeyote aliyeamini kweli kuwa mzozo huu unaweza kutatuliwa kwa kutumia mabomu, lazima abadilishe maoni yake baada ya matokeo ya juzi. Tena mapigano yanazidi kuwa mabaya. Hata tuliweza kuona jinsi watu wa kawaida walivyojitolea kuwalinda wanaharakati wa msimamo mkali kwa kujiweka kati ya Waisraeli na wanamgambo hawa. Inaonekana kuwa Israel haiwezi kuwashinda Wapalestina kwa njia ya kijeshi. Na juu ya hayo Israel inazidi kushindwa kupata uungwaji mkono kwenye jukwaa la kimataifa. Tayari watu wengi katika nchi za Magharibi wanawaunga mkono Wapalestina kwa sababu wanaonekana kuwa ni upande dhaifu dhidi ya mshindani mwenye nguvu mno kama vile inavyoandikwa katika biblia ambapo mfalme David anashindana na jitu Goliath. Yale yanayosahauliwa ni kuwa hivi juzi pia roketi zinazotumiwa na Wapalestina pia ziliwajeruhi Waisraeli raia wa kawaida wasio na hatia.”

 • Tarehe 20.11.2006
 • Mwandishi Maja Dreyer
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CHUQ
 • Tarehe 20.11.2006
 • Mwandishi Maja Dreyer
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CHUQ