1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wagombea watatu watoana jasho katika uchaguzi wa urais, Timor Mashariki.

Omar Babu9 Aprili 2007

Mshindi wa tuzo ya Nobel Jose Ramos-Horta, ambaye pia ni Waziri Mkuu, amekabiliana vikali na wagombea wengine wawili wa uchaguzi wa urais wa Timor ya Mashariki uliofanyika leo. Jose Ramos-Horta alikuwa amepigiwa upatu angeshinda uchaguzi huo moja kwa moja, lakini wadadisi wanasema awamu ya pili ya uchaguzi haitaepukika.

https://p.dw.com/p/CHGj
Rais wa Timor Mashariki anayeondoka, Xanana Gusmao.
Rais wa Timor Mashariki anayeondoka, Xanana Gusmao.Picha: AP

Waziri Mkuu, Jose Ramos-Horta, ambaye ni mshindi wa mwaka alfu moja mia tisa na tisini na sita wa tuzo ya amani ya Nobel alitaraji kuibuka na ushindi wa moja kwa moja, lakini mambo ni kinyume.

Miongoni mwa wagombea wanane waliochuana kwenye uchaguzi huo, wawili, ambao ni Francisco „Lu-Olo“ Guterres na Fernando „Lasama“ de Araujo ndio wanaoelekea kumtoa kijasho chembamba, Jose Ramos-Horta katika harakati ya kutaka kutwaa wadhifa wa urais ambao unashikiliwa na kiongozi wa zamani wa waasi, Xanana Gusmao.

Wachunguzi wamesema wapiga kura walijitokeza kwa wingi na kupiga kura kwa hali ya utulivu na amani.

Kulingana na wachunguzi hao, ni bayana kwamba kutakuwa na awamu ya pili ya uchaguzi katika nchi hiyo ambayo kabla ya uhuru wake ilitawaliwa na Indonesia kwa miongo mingi.

Kiasi watu laki tano na elfu ishirini na mbili wamesajiliwa kupiga kura katika Timor Mashariki ambayo ina vituo zaidi ya mia saba vya kupiga kura.

Ulinzi mkali ulikuwa umewekwa tangu asubuhi wapiga kura walipoanza kutunga foleni.

Hata hivyo, kuna wasiwasi kwamba hali ya mambo haitatengemaa katika nchi hiyo inayokabiliwa na misukosuko ya kisiasa.

Msemaji wa Tume ya Uchaguzi, Padre Martinho da Silva Gusmao, amesema matokeo ya awali ya uchaguzi huo yanatarajiwa kutangazwa siku ya Jumatano ingawa kwa mujibu wa taarifa kutoka vituo vya kupiga kura, Jose Ramos-Horta, alikuwa miongoni mwa wagombea waliokuwa wakiongoza.

Hapo awali, Padre Matirnho Gusmao alikuwa amezungumzia hofu aliyokuwa nayo kuhusu shughuli nzima ya uchaguzi.

"Uchaguzi huu utabadilisha tu nyuso za wakuu wa serikali. Misukosuko itabaki pale pale. Hatuna mkakati wowote uliolengwa kurekebisha hali ya mambo kwa undani"

Tume ya uchaguzi ya Timor Mashariki imesema uchaguzi huo umeendeshwa kama ulivyokuwa umepangawa na kwamba wapiga kura walijitokeza kwa wingi kuliko ilivyokuwa ikitarajiwa.

Awamu ya pili ya uchaguzi huo inatakikana kufanyika katika kipindi cha mwezi mmoja ujao.

Rais aliyeko madarakani, Xanana Gusmao, ameamua kutotetea wadhifa wake, na badala yake kusubiri uchaguzi wa bunge utakaofanyika miezi michache ijayo ili ajitose kuwania wadhifa wa Waziri Mkuu.

Jose Ramos-Horta, anayetarajiwa na wengi kushinda, awali alielezea alikuwa na imani kwamba shughuli nzima hiyo ya uchaguzi ingefana.

Mara baada ya kupata uhuru wake mwaka 2002, Timor Mashariki ilipata sifa kemkem kutokana na ari na kujitolea kwake katika ujenzi wa taifa.

Mwaka uliopita ghasia zilitibuka baada ya hatua ya aliyekuwa Waziri Mkuu, Mari Alkatiri, kuwatimua wanajeshi kadhaa.

Hatua hiyo ya waziri mkuu ilisababisha vita kati ya wanajeshi mahasimu na pia ghasia za magenge , uporaji na ukosefu wa utangamano kwa jumla.