Wafauasi wa Sadr wapiga kura ya maoni
2 Aprili 2010Wafuasi wa muungano wa vyama vya kidini vya Kishia "Iraqi National Alliance" kwa maelfu, wameanza kupiga kura ya maoni kuamua nani atakaeiongoza Iraq. Uchaguzi wa bunge uliofanywa Machi 7 haukupata mshindi wa moja kwa moja. Kura ya maoni inayopigwa leo na kesho Jumamosi haina nguvu ya kisheria. Lakini kwa wengi, hiyo ni njia inayotumiwa na Muqtada Sadr kumuunga mkono ye yote mwingine isipokuwa adui wake mkubwa, Waziri Mkuu wa hivi sasa, Nuri al-Maliki. Ili kuweza kubakia madarakani, al Maliki asiependwa na wafuasi wa Sadr, anahitaji kuungwa mkono na Washia wengi.
Chama cha Iraqiya cha Ayad Allawi kinachotenganisha dini na siasa, kimeshinda viti 91. Chama cha State of Law Alliance kinachounganisha makundi ya Kishia na kuongozwa na al-Maliki kimepata viti 89. Nafasi ya tatu imechukuliwa na Iraqi National Alliance baada ya kushinda viti 70. Hakuna aliepata wingi wa kuweza kuunda serikali peke yake. Lakini Allawi na al-Maliki wanadai kuwa na haki ya kuunda serikali mpya na hivi sasa wanajadiliana na vyama vingine. Kila mmoja wao anahangaika kuwa wa kwanza kufanikiwa kuunda serikali mpya.
Sasa, wagombea wakuu wawili, Allawi na al-Maliki, ndio wanapigania kupata kura za wafuasi wa Muqtada al Sadr katika kura ya maoni isiyo rasmi. Hata Ibrahim al-Jaafari aliekuwa waziri mkuu kabla ya al-Maliki, yupo katika orodha ya wagombea wadhifa huo. Makamu wa Rais Adel Abdel Mahdi na Jaafar al-Sadr mtoto wa mwaasisi wa chama cha al-Maliki cha "Islamic Dawa Party" vile vile ni miongoni mwa wagombea hao.
Uhasimu wa wagombea hao umevuka misingi yao ya kidini, hasa kwa sababu ya operesheni ya kijeshi ya mwaka 2008 iliyoamriwa na al-Maliki dhidi ya Jeshi la Mahdi ambalo ni tawi la kijeshi la chama cha Sadr. Matokeo ya kura ya maoni inayopigwa leo na kesho, yanatazamiwa kutangazwa siku ya Jumatatu.
Mwandishi:Martin,Prema/DPAE/AFPE
Mhariri: Othman,Miraji