1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wade asalimu amri kwa waandamanaji

24 Juni 2011

Rais wa Senegal Abdoulaye Wade amesalimu amri kuhusiana na pendekezo la mabadiliko ya sheria za uchaguzi, na kuuondoa kabisa mswada ambao ulizua vurugu kali baina ya polisi na waandamanaji katika mji mkuu Dakar hapo jana

https://p.dw.com/p/11ijn
Rais wa Senegal Abdoulaye Wade.Picha: PA/dpa

Mahasimu wa Wade walisema pendekezo hilo lingeruhusu kuchaguliwa kwake tena dhidi ya upinzani usio na nguvu katika uchaguzi ujao mwezi februari mwakani na pia lilitishia kuzuka kwa maandamano ya mapinduzi katika nchi hiyo ambayo kwa muda mrefu na uimara katika Afrika magharibi.

Kufikia jana usiku ghasia zilikuwa zimepungua lakini katikati mwa mji taswira ilikuwa ni mawe na mabaki ya magari yaliyochomwa moto. Duru ya polisi ilisema kiasi ya polisi 12 walikuwa miongoni mwa zaidi ya watu 100 waliojeruhiwa wakati wa mapambano hayo.

Wachambuzi wanasema hali hiyo pia ilionyesha jinsi upinzani pamoja na makundi ya kiraia yanavyoweza kupanga shughuli za kumpinga Wade wakati ambapo kuna hofu za kijamii nchini humo. Waziri wa sheria Cheikh Tidiane Sy aliliambia bunge kuwa rais Wade alipokea jumbe kutoka mbali hasa kutoka viongozi wa kidini, na hapo ndipo akamtaka aondoe sheria hiyo.

Awali, Wade aliondoa pendekezo la kupunguza kutoka asilimia 50 hadi 25 kiwango cha chini cha kura ambacho mgombea anahitajika kushinda awamu ya kwanza ya uchaguzi wa rais mwaka ujao..kiwango ambacho mahasimu wa Wade walisema kingemhakikishia ushindi wa mkondo wa kwanza dhidi ya upinzani wake ulio dhaifu.

Lakini vipengele vingine vilisalia, na licha ya kukubali huko, waandamanaji na wanachama wa vikosi vya usalama, wakitumia mabomu ya kutoa machozi, waliendelea kukabiliana katika maeneo yaliyo karibu na afisi za rais na bunge.

Kipengele kilichosalia chenye utata zaidi ni kile cha kuunda wadhiifa wa makamu wa rais. Mahasimu wake wanasema jukumu hilo linapendekezwa ili amkabidhi mamlaka mwanawe wa kiume Karim, ambaye tayari ni waziri mashuhuri anayesimamia robo ya bajeti ya kitaifa, lakini serikali ilisema nafasi hiyo sio lazima kwamba ingechukuliwa na Karim.

Ibrahima Sene, afisa wa ngazi ya juu wa muungano wa upinzani wa Benno Siggil nchini Senegal, aliwasifu waandamanaji kwa kujitolea kwao lakini akasema walifanya kazi nusu tu. Amesema bado kuna kazi ya kumwondoa Wade madarakani, na huo ndio mwito wanaotoa.

Senegal imetambulika kwa muda mrefu kama taifa lililo imara zaidi na lenye demokrasia Afrika Magharibi na limeshuhudia chaguzi kadhaa zenye amani kwa miaka 50 iliyopita tangu ilipopata uhuru wake kutoka Ufaransa. Lakini kuna ongezeko la wasiwasi kuhusu kupewa madaraka mengi washirika wa karibu wa rais Wade, pamoja na raia kukata tamaa kutokana na kuzorota kwa huduma za umma na kupanda kwa bei za bidhaa muhimu.

Mwandishi: Bruce Amani/Reuters

Mhariri: Abdul-Rahman,Mohammed