1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wasiwasi miongoni mwa wanariadha wa Kenya

20 Novemba 2015

Sio Urusi tu ambako kuna kitisho cha wanariadha wake kufungiwa katika Michezo ya Olimpiki. Kuna wasiwasi pia miongoni mwa wanariadha wa Kenya kwamba huenda hatua kama hiyo ikachukuliwa dhidi ya Kenya.

https://p.dw.com/p/1H9ZU
Chicago Marathon 2013 Rita Jeptoo
Picha: picture-alliance/dpa/Tannen Maury

Hii ni baada ya Rais wa Kamati ya Olimpiki ya Kenya, Kipchoge Keino kuonya kuwa WADA inatafakari kuipiga Kenya marufuku kwa miaka minne, ikiwa ni pamoja na Michezo ya Olimpiki. Keino hata hivyo anasema kamati yake ya Olimpiki haina matatizo yoyote ya matumizi ya dawa hizo kwa sababu wanafanya vipimo vya mara kwa mara.

Bingwa wa zamani wa mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji Moses Kiptanui anasema hali hiyo ni ngumu maana inawaathiri wachezaji ambao ni safi "Tunapaswa kuona mchezo ambao mshindi anashinda kwa haki. AK inapaswa kuwajibika lakini hata nikisema AK, kesi hiyo imefikia shirika la kimataifa la IAAF. Ikiwa kiongozi wa juu ni mfisadi, nini kitawazuiwa samaki wadogo kuoza? Ikiwa kiongozi wa juu ameoza, vipi kuhusu kiongozi wa chini? Ni mbaya hata zaidi".

Mapema mwaka huu gazeti la Uingereza la Sunday Times na Televisheni ya Ujerumani ARD/WDR waliripoti kuwa baadhi ya wanariadha wa Kenya walikuwa na matokeo ya ya kutilia shaka ya vipimo vya kuonyesha matumizi ya dawa zilizopigwa marufuku. Wanariadha wengi wanasema kukithiri kwa ufisadi ndani ya Chama cha Riadha cha Kenya ndiko kunakosababisha mgogoro wa matumizi ya dawa za kuongeza misuli nguvu.

Lakini Afisa mkuu wa AK Isaac Mwangi anakanusha madai hayo akisema tatizo walilonalo ni ukosefu wa ufadhili wa kutosha "Kama Athletics Kenya, sera yetu ni wazi kabisa, hatukubali matumizi ya dawa za kusisimua misuli, hatutamficha yeyote anayepatikana na hatia. Bila shaka tunapaswa kuwapa fursa ya kusikia upande wao wa mambo lakini muhimu ni kuwa sheria zetu haziruhusu tabia hiyo na yeyote atakayepatikana hana njia nyingine. Tutamtaja na kumwondoa mashindanoni. Hatutamruhusu mtu kuharibu sifa nzuri ya nchi hii".

Baada ya kuchoshwa na kile wanahisi kuwa ni usimamizi mbaya wa Chama cha Riadha Kenya, wanariadha kadhaa nguli nchini Kenya walichukua hatua na kuunda Muungano wa Wanariadha wa Kulipwa wa Kenya – PAAK na kwa usaidizi wa WADA, wameanza kuandaa warsha za kuelimisha kuhusu dawa za kuongeza nguvu mwilini miongoni mwa wanariadha na kushirikiana na maduka ya dawa ya nchini humo ili kuwazuia wanariadha kutumia dawa hizo zilizopigwa marufuku.

Serikali imesema itaimarisha juhudi za Shirika la Kenya la Kupambana na Matumizi ya Dawa za kuongeza misuli nguvu – ADAK ambalo lilianzishwa mara ya kwanza mwaka wa 2013.

Mwandishi: Bruce Amani/DPA/AFP/AP/Reuters
Mhariri:Yusuf Saumu