Waasi watangaza taifa la Kiislam kaskazini mwa Mali | Matukio ya Afrika | DW | 28.05.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Afrika

Waasi watangaza taifa la Kiislam kaskazini mwa Mali

Waasi wa Tuareg na kundi la Kiislam la Ansar Diin wametangaza kuunda taifa jipya la Kiislam la Azawad kaskazini mwa Mali katika makubaliano yaliyofikiwa siku ya Jumapili.

Wanajeshi wa jeshi la MNLA wakifanya doria kaskazini mwa Mali.

Wanajeshi wa jeshi la MNLA wakifanya doria kaskazini mwa Mali.

Tangazo hili limekuja wakati rais wa muda wa Mali yuko nchini Ufaransa kwa matibabu baada ya kupigwa na raia wenye hasira wiki iliyopita kufuatia makubaliano yaliyoiongezea serikali ya mpito muda wa miezi 12.

Kanali Bouna Attwayib ambaye ni kamanda wa Vuguvugu la Ukombozi wa Azawadi (MNLA) aliiambia BBC kuwa ni kweli makundi hayo mawili yamefikia muafaka na kwamba Azawadi sasa ni taifa huru na litakaloendeshwa kwa misingi ya Uislam.

Moussa Ag Assarid, mmoja wa viongozi wa Chama cha MNLA.

Moussa Ag Assarid, mmoja wa viongozi wa Chama cha MNLA.

Makubaliano kati ya MNLA na Ansar Diin yalisainiwa katika mji wa Gao ambao ulichukuliwa na waasi mwezi Aprili pamoja na ile ya Kidal na Timbuktu. Chama cha Ukombozi wa Azawad kilianzisha harakati za ukombozi na kuungwa mkono na Ansar Diin na baada ya kuyashinda majeshi ya serikali, Ansar diin walitangaza mpango wa kuanzisha utawala wa sharia ambao ulipingwa na MNLA.

Lakini katika tangazo lao la Jumapili, Ansar Diin na MNLA walisema wote wanakubaliana na uhuru wa Azawad na pia wote wanaukubali Uislam kama diin na kwamba diin hiyo ndiyo itakuwa mhimili wa sheria. Serikali yas Mali ambayo inakabiliwa na changamoto lukuki imepinga madai hayo ya MNLA na Ansar Diin.

Serikali ya mpito, ECOWAS wapinga kugawanywa Mali
Waziri wa Mawasiliano katika serikali ya mpito Hamadoun Toure amasema serikali yake inapinga vikali wazo la kuunda taifa la Azawad na hasa la Kiislam hata kama uundwaji huu ni wa kwenye makaratasi tu. Toure amesisitiza kuwa Mali ni nchi isiyoegemea diin na itabaki hivyo.

Nayo Jumuiya ya kiuchumi ya Mataifa ya magharibi ECOWAS ambao ndiyo wasuluhishi wa mgogoro huo imesema inapinga vikali kugawanywa kwa taifa la mali na kuwataka MNLA na Ansr Diin wakubali kuzungumza na utawala mjini Bamako na kuonya kuwa japokuwa waasi hao wanadhibiti maeneo yalio na raia, lakini hawana udhibiti wa eneo lote.

Akiongea na Televisheni ya Al Jazeera, Mkurungenzi wa masuala ya siasa wa ECOWAS Abdul Fatau Musah alisema: "Tutawafukuza katika maeneo yote haya yenye wakaazi, na tuna uwezo wa kufanya hivyo. Jeshi la ECOWAS limejipanga na tunakamilisha tu maandalizi. Wasipokubali suluhu kwa njia ya mazungumzo huko kaskazini, basi tutatumia njia nyengine kuwalaazimisha."

Mfugaji wa Kituareg akisimama mbele ya msikiti wa karne ya 13 mjini Timbuktu.

Mfugaji wa Kituareg akisimama mbele ya msikiti wa karne ya 13 mjini Timbuktu.

Tuareg walipata nguvu kutoka kwa Ghadaffi
Waasi wa Tuareg ambao wengi wao walikuwa mamluki katika jeshi la aliyekuwa kiongozi wa Libya Kanali Muammar Ghadafi, walirudi makwao wakiwa na zana nzito za kivita na kuanzisha mapambano katikati ya mwezi Januari. Mapinduzi yaliyoongozwa na Kapteni Amadou Sanogo yaliiangusha serikali mjini Bamako tarehe 22 Machi kwa madai kuwa ilikuwa imeshindwa kushughulikia tatizo la waasi wa Tuareg.

Lakini mapinduzi haya yalizidi kufungua njia kwa waasi wa Tuareg, Ansar Diin kujizatiti katika eneo hilo la kaskazini ambalo ni kubwa kuliko Ufaransa. Viongozi wa serikali ya mpito mjini Bamako wamesisitiza nia yao ya kurejesha utawala kaskazini lakini hata wao wameshindwa kuhakikisha usalama wao wenyewe, achilia mbali kuthubutu kukabiliana na watawala wapya kaskazini.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/AFPE/DPAE
Mhariri: Mohamed Khelef