1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi wa zamani Cote d'Ivoire wapandishwa vyeo

Iddi Ssessanga
27 Januari 2017

Rais wa Cote d'Ivoire amewapandisha vyeo makamanda wawili wa zamani wa waasi waliounga mkono upande wa serikali katika mazungumzo ya kuzima uasi wa wanajeshi mapema mwezi Januari.

https://p.dw.com/p/2WWLS
Elfenbeinküste Militär trifft sich im Flughafen von Bouake
Luten Kanali Issiaka Outtara (kushoto) akizungumza na Luteni Kanali Harve Toure Armand Pelikan katika uwanja wa ndege wa Bouake Januari 13,2017. Outtara sasa ndiye kamanda wa kikosi cha ulinzi wa Jamhuri.Picha: Reuters/T. Gouegnon

Ofisi ya Rais Alassane Ouattara ilitangaza Alhamisi jioni kwamba Luteni Kanali Issiaka Outtara angeongoza kitengo chenye nguvu cha Ulinzi wa Jamhuri, ambako alikuwa naibu kamanda. Pia ilisema Luteni Kanali Cherif Ousmane atatoka kwenye kikosi cha ulinzi wa rais na kuongoza kitengo cha makomando.

Wawili hao walikuwa makamanda wa waasi wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyoigawa Cote d'Ivoire katika pande mbili kuanzia 2002 hadi 2011. Pia walikuwa watu muhimu katika mgogoro wa 2011 uliomuingiza Outtara madarakani baada ya mpinzani wake, rais wa zamani Laurent Gbagbo, kukataa kukabidhi madaraka. Mapambano hayo ya madaraka yalisababisha vifo vya watu 3,000.

Januari 6, waasi wa zamani waliogeuka wanajeshi mjini Bouake, ambao ni mji mkuu wa zamani wa waasi, waliasi kuhusiana na malalamiko yakiwemo kutolipwa bakhsishi zao waliozoahidiwa kutokana na mchango wao katika mgogoro huo. Uasi huo ulisambaa haraka katika miji mingine, ukiwemo mju mkuu wa kibishara Abidjan.

Wakosoaji wakasirishwa

Issiaka Outtara na Ousmane walijiunga na ujumbe wa serikali, ulioongozwa na waziri wa ulinzi Alain-Richard Donwahi, uliojadiliana makubaliano yanayohusisha malipo makubwa. Waasi walisema serikali ilikubali kulipa bakhshishi za karibu dola 20,000 kwa wanajeshi zaidi ya 8,000, ingawa serikali haijathibitisha kiasi hicho cha pesa.

Kufuatia makubaliano hayo, Donwahi aliahidi kurejesha udhibiti wa jeshi lake ili litowe huduma ya kweli kwa taifa. Lakini upandishaji huo wa vyeo una uhakika wa kuwakasirisha wakosoaji wa serikali wanaoilaumu kwa kushindwa kuwadhibiti makamanda wa zamani wa waasi.

Mwaka 2011, shirika la kutetea haki za binaadamu la Huma Rights Watch lilimuorodhesha Ousmane kama mmoja wa wapiganaji wanaomuunga mkono Outtara waliotajwa kuhusika katika uhalifu mkubwa wakati wa mgogoro wa baada ya uchaguzi.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/ape

Mhariri: Saumu Yusuf