1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waangalizi kuzuru vitovu vya maandamano Idlib, Daraa, na Hama nchini Syria

28 Desemba 2011

Mkuu wa kundi la waangalizi la Umoja wa nchi za Kiarabu, Arab League, nchini Syria amesema ana matumaini kuhusu ujumbe wake unaolenga kumaliza miezi tisa ya michafuko nchini humo.

https://p.dw.com/p/13aWh
Mojawapo ya mabango yenye picha ya Rais wa Syria Bashar al Assad yakiashiria kuupinga utawala wake
Mojawapo ya mabango yenye picha ya Rais wa Syria Bashar al Assad yakiashiria kuupinga utawala wakePicha: dapd

Mohammed Ahmed Musrafa al Dabi, jenerali mkongwe katika jeshi la Sudan, ambaye anaongoza ujumbe wa waangalizi wa jumuiya ya Kiarabu nchini Syria, ameliambia gazeti la Al Hayat la mjini London kuwa kufikia sasa serikali ya Syria, imeshirikiana nao, lakini hawatatoa maelezo ya ripoti yao kwa waandishi wa habari.

Dabi anasema sehemu kadhaa za mji unaokumbwa na makabiliano, Homs, zilikuwa katika hali mbaya, lakini wajumbe hawakuona chochote cha kuogofya maanake kulikuwa na utulivu na hakukuwa na mapigano.

Alisema tayari amekutana na waziri wa mambo ya nchi za nje wa Syria, Walid al -Muallem, na kwamba atakutana na maafisa wengine. Dabi aliongeza kuwa mambo kwa sasa yanaonekana kwenda sawa na wanatumai kupiga hatua za manufaa katika shughuli yao, akidokeza kuwa ujumbe huo ulikuwa wa kwanza wa aina yake katika historia ya umoja wa Kiarabu.

Tovuti ya Syria News wakati huo huo imemnukuu Dabi akisema kuwa waangalizi hao ambao jana walizuru mji wa kati ambao ni kitovu cha ghasia, Homs, walikusanya maoni kutoka kwa pande zote husika.

Televisheni ya Syria Al Dunia iliripoti leo kuwa waangalizi hao watasafiri hadi maeneo yalikozuka maandamano ya Hama na Idlib karibu na mpaka wa Uturuki, ijapokuwa haikutoa ratiba ya ziara hiyo.

Jukumu kuu la waangalizi hao ni kusimamia utekelezaji wa mpango ulioundwa na jumuiya ya nchi za kiarabu unaotaka kuondoka kwa vikosi vya usalama katika maeneo yanayokaliwa na raia na kuwachiliwa huru watu waliokamatwa wakati wa vurugu hizo.

Katibu mkuu wa umoja wa nchi za Kiarabu, Nabil al- Arabi, anasema serikali ya Syria inafaa kushirikiana na waangalizi.

Kwingineko shirika la kutetea haki za binadam la HUMAN Rights Watch limeushtumu utawala wa Syria kwa kuwaficha mamia ya wafungwa waliokamatwa kwenye msako wa waandamanaji. Shirika hilo lilisema wafungwa hao huenda wamehamishwa kisiri hadi kambi za kijeshi ili kuwaficha wasionekane na waangalizi wa jumuiya ya kiarabu. Sasa shirika hilo limeitaka jumui ya kiarabu kuhakikisha wajumbe wake wanazuru maeneo yote yaliyotumiwa kuwazuilia waandamanaji jinsi mkataba uliofakiwa baina yake na serikali ya Syria unavyosema.

Mji wa Homs ambao umeshuhudia ghasia mbaya katika siku za hivi karibuni
Mji wa Homs ambao umeshuhudia ghasia mbaya katika siku za hivi karibuniPicha: dapd

Huku hayo yakijrii, wanaharakati wanatilia shaka uwezo wa kiongozi wa kundi hilo la waangalizi wa kusaidia kutatua mgogoro wa Syria. Wanasema Luteni Jenerali Mustafa al Dabi kutoka Sudan hangepewa jukumu la kuuongoza ujumbe huo, ikizingatiwa kuwa Sudan ilikataa kuwa mwanachama wa mahakama ya kimataifa ya ICC, na hivyo huenda asichukue hatua thabiti dhidi ya rais wa Syria Bashaar al Assad.

Lakini nao umoja wa nchi za kiarabu ´unasema Dabi ana ujuzi na ufahamu wa kijeshi na kidiplomasia unaoweza kuusaidia ujumbe huo kuthibitisha kuwa Assad anatekeleza mpango wa kumaliza ukandamizaji dhidi ya waandamanaji.

Mwandishi: Bruce Amani DPA/AFP

Mhariri: Miraji Othman