1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waangalizi kukutana na Waziri wa Nje wa Syria

Martin,Prema/afpe/rtre24 Desemba 2011

Wajumbe wa Umoja wa Nchi za Kiarabu leo wanatazamia kukutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria Walid Muallem, kama sehemu ya makubaliano ya kuumaliza umwagaji damu nchini humo

https://p.dw.com/p/13YkH
People stand at the site of a suicide bombing in Damascus, Syria, Friday, Dec. 23, 2011. A Syrian military official says the death toll from twin suicide car bombings in Damascus is now more dozens. The military official says more than a hundred people were wounded in the explosions targeting security and intelligence headquarters in the Syrian capital. (Foto:Muzaffar Salman/AP/dapd)
Machafuko yapamba moto SyriaPicha: dapd

Machafuko hayo yalichukua mkondo mpya siku ya Ijumaa baada ya washambuliaji wa kujitoa mhanga kuwaua watu 44 katika mji mkuu Damascus. Wengine 166 walijeruhiwa katika mashambulio hayo mawili yaliyoyalenga majengo ya idara ya upelelezi na usalama. Serikali imewalaumu wanamgambo wa al-Qaeda, lakini Baraza la Taifa la Syria linalojumuisha makundi ya upinzani linadai kuwa serikali ndio inayobeba jukumu la mashambulio hayo ya kigaidi. Baraza hilo limesema, serikali inautaka ulimwengu uamini kuwa Syria inakabiliwa na kitisho kutoka nje na sio mapinduzi maarufu ya umma unaodai uhuru na heshima. Mashambulio ya jana yamelaaniwa pia na Umoja wa Mataifa.

Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon amesema, Ban ana wasiwasi na machafuko yanayozidi kupamba moto nchini Syria. Ameihimiza serikali kuutekeleza haraka na kikamilifu mpango wa amani uliopendekezwa na Umoja wa Nchi za Kiarabu. Kuambatana na mpango huo, Syria inapaswa kuyaondosha majeshi kutoka miji iliyo ngome za upinzani, kusitisha mashambulio dhidi ya raia, kuwaachilia wale waliowekwa kizuizini na kuanzisha majadiliano pamoja na upinzani. Wakati huo huo,msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani, Mark Toner amesema Marekani inalaani vikali kabisa mashambulio yaliyofanywa Damascus hapo jana. Akaongezea kuwa ni muhimu kuhakikisha kuwa mashambulio hayo hayatokwamisha kazi muhimu ya wajumbe wa Umoja wa Nchi za Kiarabu.

Wajumbe hao wanafanya matayarisho ya kimiundo mbinu kwa ajili ya kundi la kwanza la waangalizi linalojumuisha zaidi ya wataalamu 50 wa masuala ya kisiasa, kijeshi, haki za binadamu, na usimamizi wa migogoro. Hatimae idadi ya wataalamu hao itafikia 150 hadi 200. Kundi la kwanza la wataalamu hao litakwenda Syria siku ya Jumatatu, kama sehemu ya makubaliano yaliyofikiwa Novemba 2 pamoja na Syria. Lakini viongozi wa upinzani wanasema, Syria imeuukubali mpango huo ili kuuzuia Umoja wa Nchi za Kiarabu kulifikisha suala la Syria katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusiana na ukandamizaji wa upinzani unaofanywa na vikosi vya usalama nchini humo.

Wakati huo huo, nchi za Ulaya na Marekani zinatoa mwito kwa Baraza la Usalama kuiwekea Syria vikwazo vikali zaidi kwa sababu ya ukandamizaji wa upinzani unaoendelea nchini humo tangu miezi tisa. Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, zaidi ya watu 5,000 wameuawa tangu maandamano ya upinzani yalipoanza mwezi wa Machi nchini humo. Nchi za magharibi zinasema vikosi vya serikali ndio vilivyohusika na sehemu kubwa ya umwagaji damu huo.