1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waandishi Uganda wapinga hujuma za jeshi dhidi yao

28 Desemba 2020

Wandishi habari Uganda wamesusia kikao cha vyombo vya usalama kupinga hujuma dhidi yao inayofanywa na majeshi ya serikali. Ijapokuwa mratibu wa masuala ya kisiasa wa jeshi ameahidi kuwahakikishia usalama wao.

https://p.dw.com/p/3nHCi
Uganda | Journalisten am Uganda Media Center
Picha: Lubega Emmanuel/DW

Katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu, wanahabari wameelezea kuhisi kupuuzwa kwani amesita kutamka neno lolote la kuomba radhi kuhusu visa vya jana ambapo wanahabari watatu walijeruhiwa na wako mahututi. 

Polisi imeitwa mara moja kwenye kituo cha serikali cha habari kudhibiti hali pale wanahabari walipoanza kupaza sauti za kuvishtumu vyombo vy usalama kwa mienendo yao ya kuwashambulia wakifanya kazi zao.

Hii ni kutokana na visa vya jana ambapo waandishi habari watatu walijeruhiwa katika vurugu zilizozuka wakati wajeshi na polisi walipojaribu kuwasambaratisha wafuasi wa mgombea urais wa upinzani Robert Kyagulanyi.

Waandishi wamekosolewa kwa kukosa uzalendo

Mmoja kati ya waandishi habari waliojeruhiwa vibaya ni Ashraf Kasirye ambaye huwa katika msafara wa mgombea urais Robert Kyagulanyi, amejeruhiwa na yuko mahututi kutokana na ghasia za jana. Kasirye alipigwa risasi ya mpira kichwani.

Uganda Oppositionsführer und Rapper Bobi Wine
Mwanasiasa wa upinzani Uganda Bobi WinePicha: Ronald Kabuubi/AP/picture alliance

Waandishi habari walitarajia mratibu wa masuala ya kisiasa wa majeshi Jenerali Henry Matsiko kutanguliza tamko la kuomba radhi, lakini badala yake amewakosoa kwa kutokuwa na moyo wa uzalendo na kuonyesha upendeleo wa upande mmoja.

Vitendo vya jeshi la polisi kuwahujumu waandishi habari vimeongezeka katika kipindi hiki cha kampeni za uchaguzi wa rais ambapo hadi sasa wanahabari 15 wameshambuliwa wakiwa kazini na vifaa vyao kuharibiwa.

Upinzani umeikosoa Tume ya Uchaguzi Uganda

Vitendo hivi vimekemewa vikali na watu mbalimbali ikiwemo mabalozi na jumuia ya kimataifa. Manyanyaso haya yamewakumba hata waandishi habari wa kimataifa ambao baadhi yao wamezuiliwa kuja Uganda kufuatilia uuchaguzi utakaofanyika tarehe 14 mwezi ujao wa Januari.

Afrika | Kenia Uganda Proteste  Bobi Wine Opposition
Wafuasi wa Bobi Wine wakiandamanaPicha: AP Photo/picture alliance

Wakati huo huo, wagombea wa vyama vyote wameikosoa Tume ya Uchaguzi kutangaza kusimamisha kampeni katika miji 13 kwa madai kuwa miji hiyo inakumbwa na ongezeko la maambukizi ya COVID-19.

Kinachosangaza ni kwamba tume imeshauri kuwa kampeni zifanyike kupitia vyombo vya habari. Lakini kulingana na uhasama ambao umeibuka kati ya utawala na wadau katika uandishi habari kuna mashaka kama hili litafanyika ipasavyo.