1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waandishi habari waandamwa Misri.

Mohamed Dahman27 Oktoba 2007

Serikali ya Misri imeimarisha kampeni yake dhidi ya vyombo huru vya habari na vile vya upinzani kwa mahkama za jinai kuwahukumu vifungo gerezani waandishi habari mashuhuri 12 katika kipindi cha miezi miwili iliopita.

https://p.dw.com/p/C7g8
Rais Housni Mubarak wa Misri kufungwa gerezani kwa waandishi wa habari nchini mwake kunaweza kuathiri mageuzi ya kisiasa na uchumi nchini humo.
Rais Housni Mubarak wa Misri kufungwa gerezani kwa waandishi wa habari nchini mwake kunaweza kuathiri mageuzi ya kisiasa na uchumi nchini humo.Picha: dpa

Wakati waendesha mashtaka wa serikali wanawashutumu waandishi habari kwa kuchapisha habari za uongo shirika la waandishi wa habari nchini humo linasema hivyo ni vita dhidi ya uhuru wa vyombo vya habari.

Yahia Qulash katibu mkuu wa Shirika la Waandishi Habari nchini Misri la Egypt Journalists Syndicate ameliambia shirika la habari la IPS kwamba kuandamwa huko kwa vyonbo vya habari ni thibitisho kwamba utawala wa nchi hiyo umeshindwa kuwavumilia waandishi habari wachache wa kujitegemea ambao wamediriki kuishutumu serikali.

Kampeni hiyo ilianza tarehe 13 mwezi wa Septemba wakati wahariri wakuu wa magazeti mashuri manne yalio huru walipohukumiwa kifungo cha mwaka mmoja gerezani kila mmoja wao kwa kuchapisha habari za kukashifu juu ya Rais Housni Mubarak na wanachama wengine mashuhuri wa chama chake tawala cha National Demokratik NDP.

Muda mfupi baada ya hapo yaani hapo tarehe 24 mwezi wa Septemba mhariri mkuu na waandishi habari wawili kutoka gazeti la kila siku la upinzani wa kiliberali la al –Wafd wameonekana kuwa na hatia kwa kuchapisha taarifa za uzushi hapo mwezi wa Januari ambazo imeelezwa kuwa chanzo chake kilikuwa wizara ya sheria. Katika kesi hii washtakiwa watatu kila mmoja alihukumiwa miaka miwili gerezani.

Vyombo huru vya habari vikaja kupata pigo jengine baada ya hapo kutokana na wafanyakazi saba wengine wa gazeti la Saout al Umma kuhukumiwa vifungo vya kati ya mwezi mmoja hadi miezi miwili kutokana na kesi mbili tafauti za kuchapisha habari za uongo.

Mhariri mkuu wa gazeti la al Dastour Ibrahim Eissa ambaye ni mkosoaji wa muda mrefu wa sera za serikali pia anakabiliwa na shutuma za kuchapisha habari za uongo kuhusu suala nyeti la afya ya Rais.Iwapo atapatikana na hatia anaweza kukabiliwa na kifungo cha hadi miaka minne gerezani ikiwa ni ziada ya kutozwa faini kubwa za fedha.

Kwa mujibu wa waendesha mashtaka Eissa alikwenda kinyume na utashi wa wananchi wakati alipotowa repoti hapo mwezi wa Augusti yenye kudokeza kwamba Mubarak mwenye umri wa miaka 79 alikuwa mgonjwa mahtuti.Waendesha mashtaka wanadai kwamba uvumi huo ambao ulikuja kuthibitika kuwa sio kweli ulisababisha kuondolewa kwa vitega uchumi vya kigeni kwenye uchumi wa ndani ya nchi na kuanguka sana kwa masoko ya hisa.

Hapo mwaka 2004 Rais Mubarak aliahidi kuzifanyia marekebisho sheria za vyombo vya habari kwa nia ya kutokomeza utaratibu wa hukumu za vifungo gerezani kwa makosa ya uchapishaji lakini licha ya ahadi hiyo sheria kali zinaendelea kubakia pale pale na waandishi habari bado wanakabiliwa na hatari ya kutumikia vifungo gerezani kwa kuchapisha mambo yanayoonekana kuukosowa mno uongozi wa serikali.

Eissa awali alikuwa ashtakiwe na mahkama ya usalama wa taifa ambapo hukumu zake kinyume na mahkama za kiraia huwa hazina rufaa lakini baada ya wimbi la shutuma kutoka makundi ya haki za binaadamu na uhuru wa kiraia ya ndani ya nchi na nje ya nchi serikali ilibadili mkondo wake na kutangaza kwamba kesi hiyo itaendeshwa kwenye mahkama ya kiraia.

Kuongezeka kwa vyombo huru vya habari nchini Misri kunawakilisha mojawapo ya mafanikio machache ya hivi karibuni kuhusiana na suala la kuifunguwa nchi hiyo ambapo mara nyingi imekuwa ikitajwa kuwa ni ushahidi wa kujizatiti kwa nchi hiyo katika mageuzi ya kisiasa yaliopelekea kuongezeka kwa uwekezaji wa kigeni.

Wana habari wa kujitegemea wanaona kutupwa gerezani kwa waandishi wa habari yumkini kukawa na taathira ya hatari kisiasa na kiuchumi kwa nchi nzima.