″Vuguvugu jipya la amani nchini Marekani? - Hapana!″ | Magazetini | DW | 19.03.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Magazetini

"Vuguvugu jipya la amani nchini Marekani? - Hapana!"

Wikiendi iliyopita siasa pirika piriza za kisiasa kazijattulia. Kule Palestina, serikali mpya imeapishwa, Marekani kulifanyika maandamano dhidi ya vita vya Iraq na Kansela wa Ujerumani alimaliza ziara yake nchini Poland ambapo suala la mitambo ya Wamarekani ya kufyetua makombora linaendelea kuzusha mijadala mikali. Hayo yote yamo katika udondozi wa magazeti.

Tunaanza na kuapishwa serikali mpya ya Wapalestina. Mhariri wa gazeti la “Frankfurter Allgemeine” ameandika kuwa serikali hii ya umoja ni ishara ya nguvu ya chama cha Hamas na pia inaonyesha udhaifu wa Fatah. Hamas kinaongoza katika serikali hii, hata hakikulazimika kulitambua taifa la Israel. Na mhariri huyu anaendelea kusema kuwa pande zote mbili hazikuwa na chaguo jingine, kwa vile mvutano wa kuwa na mamlaka uliziathiri mno.

“Je, serikali hii mpya ya Palestina inafaa kususiwa kama ile ya awali ya Hamas? - anauliza mhariri wa gazeti la “Frankfurter Rundschau”. Na anaichambua hali hivi: “Tayari serikali za Ulaya zinafikiria kama kuna njia ya tatu kati ya kuitenganisha serikali hii na kuwa na uhusiano wa kawaida. Kuna hoja kuwa dai la kuitambua Israel lisiachwe. Lakini mara nyingine kushawishi ni bora kuliko kushinikiza. Na hoja nyingine ni ya kwamba mbali na mawaziri wa chama cha Hamas kuna wengine wanaounga mkono kuwepo kwa nchi mbili, Palestina na Israel.” - ni gazeti la Frankfurter Rundschau.

Gazeti la “Tageszeitung” la mjini Berlin linazungumzia maandamano dhidi ya vita vya Iraq yaliyofanywa nchini Marekani na linauliza: “Je, hilo ni vuguvugu jipya la amani nchini Marekani? Kwa bahati mbaya si hivyo, bali wanaharakati hawa hawana nguvu. Ili kuhakikisha kuwepo kwa idadi kubwa ya waandamanaji walichagua siku ambapo miaka 40 iliyopita kulifanywa maandamano dhidi ya vita vya Vietnam. Lakini hata hivyo, matokeo yake ni duni mno.” - ameandika mhariri wa “Tageszeitung”.

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani, amemaliza ziara yake nchini Poland juzi ambapo wakati wa mkutano wa pamoja na viongozi wa nchi hiyo jirani ya Ujerumani alizungumzia pia mitambo ya Marekani ya kufyetua makombora inayopangwa kujengwa nchini Poland na Tchechnia. Suala hilo litazungumziwa pia katika bunge la Ujerumani leo hii. Mitambo hiyo inapingwa hasa na serikali ya Urusi. Kabla ya ziara yake huko inayoanza hii leo mjii Washington, waziri wa nchi za nje wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier alionya dhidi ya mashindano mengine ya kulengeneza silaha. Mhariri wa gazeti la “Die Welt” lakini anashangaa juu ya maneno haya makali. Ameandika:
“Mashindano ya silaha? Hapana, zaidi ni mashindano ya kutoelewana katika mvutano huu juu ya mtambo wa kufyetua makombora. Hivyo nchi za Magharibi zinajiathiri wenyewe. Marekani, kwa upande wake, imeshakata tamaa kuzuia silaha za kinyuklia nchini Iran na ndiyo maana inataka kujenga mfumo wa kujilinda. Poland inaonekana kutaka kuwa ni mkoa wa Marekani. Warusi wanatumia fursa hii kuutenganisha Umoja wa Ulaya na jumuiya ya NATO. Iran lakini itakuwa mshindi wa mvutano huu.” - huu ni uchambuzi wa gazeti la “Die Welt”.

Na mwishowe tunalinukuu gazeti la “Stuttgarter Zeitung” kuhusu suala hilo:
“Si kwa maslahi ya Ulaya Urusi inapowa na hofu. Ni kweli kuwa Ulaya inategemea nishati ya kutoka Urusi. Lakini hata bila ya kujali masuala ya nishati, lazima Urusi isitengwe. Si lazima kuzipenda sera za rais Vladimir Putin wa Urusi, lakini ni jukumu la Ujerumani kuijumisha Urusi katika masuala ya Ulaya na kusaidia kutoa mashaka pande zote husika.”

 • Tarehe 19.03.2007
 • Mwandishi Maja Dreyer
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CHTT
 • Tarehe 19.03.2007
 • Mwandishi Maja Dreyer
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CHTT