1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vita vya Iraq: Tony Blair aomba radhi

7 Julai 2016

Ripoti ya Sir John Chilcot imebainisha kwamba vita vya Irak vilikuwa vya makosa. Kwa mujibu wa ripoti hiyo vita hivyo havikupaswa kuwa suluhisho la mwisho la mgogoro

https://p.dw.com/p/1JKxP
Waandamana kumshutumu Blair kwa vita vya Iraq
Waandamana kumshutumu Blair kwa vita vya IraqPicha: Getty Images/D. Kitwood

Aliekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza Tony Blair aliitumbukiza nchi yake katika vita vya nchini Iraq bila ya maandalizi mazuri. Aidha vita hivyo vya mwaka wa 2003 vilikuwa vya mashaka kisheria. Ripoti iliyotolewa leo juu ya vita hivyo vilivyoongozwa na Marekani imezibainisha kasoro hizo.

Ripoti hiyo inayoitwa ya Sir John Chilcot pia imebainisha kwamba uamuzi wa Uingereza wa kuungana na Marekani katika kuivamia Iraq ulichukuliwa kabla ya kuzitafakari njia nyingine zote, na kwamba uamuzi huo ulikiwamo katika msingi wa upelelezi potofu.

Akihutubnia bungeni baada ya ripoti hiyo kutolewa hadharani, Waziri Mkuu wa sasa wa Uingereza David Cameron amesema inapasa kujifunza kutokana na makosa ya mgogoro huo wa Iraq.

Cameron ameeleza kuwa sasa pana taratibu mahsusi za kutathmini taarifa za kijasusi na njia ya kuzitumia taarifa hizo.

Großbritannien Tod von Jo Cox - Jeremy Corbyn Labour Führer
Kiongozi wa chama cha "Leba" nchini Uingereza Jeremy CorbynPicha: picture-alliance/PA Wire/P. Toscano

Nchi kadhaa zilishirikiana na Marekani katika kuivamia Irak kwa kisingizio kwamba Saddam Hussein alikuwa nazo silaha za maangamizi. Lakini Waziri Mkuu Cameron amekiri kwamba kwamba kilichokuwa kinatuhumiwa kwa muda mrefu hakikuakisi ukweli wa mambo.Amesema hapakuwapo na msingi wowote wa kuonyesha kwamba Iraq ilikuwa inasababisha hatari yoyote.

Blair akubali kuwajibika

Aliekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza wakati wa vita vya Iraq Tony Blair amesema anazikubali lawama zilizotolewa juu ya vita hivyo katika ripoti ya Sir John Chilcot.

Lakini amejijitetea kwa kueleza kwamba dunia ilikuwa na itaendelea kuwa ya usalama zaidi bila ya kuwepo Saddam Huusein. Blair amesema aliupitisha uamuzi wa kwenda vitani nchini Iraq,pamoja na Marekani, kwa sababu aliamini kwamba uamuzi huo ulikuwa sahihi.

Blair amesema hakuwa na chaguo la kuuchelewesha uvamizi na kwa ajili hiyo ameomba radhi.

Hata hivyo Kiongozi wa chama cha upinzani cha Labour nchini Uingereza Jeremy Corbyn ameitaka nchi yake iwe na uhuru na kwamba pawepo uwazi , katika uhusiano wake na Marekani ili kuepusha uvamizi kama ule uliofanywa nchini Iraq ambao amesema kilikuwa kitendo cha kihalifu.

Bwana Corbyn pia amesisitiza ku wa vita vya nchini Iraq havikupaswa kuwa njia ya mwisho ya kuutatua mgogoro. Ameitaka Uingereza izingatie sheria za kimataifa na iheshimu mamlaka ya Umoja wa Mataifa.

Lakini watu wa Iraq wamesema hawakuridhishwa na ripoti hiyo kwa sababu haikushauri juu ya Waziri Mkuu wa zamani Tony Blair kufunguliwa mashtaka. Watu wa Iraq zaidi ya 150,000 na wanajeshi wa Uingereza 179 walikufa katika vita hivyo.

Mwandishi:Mtullya Abdu/rtre, afp.
Mhariri:Iddi Ssessanga