1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vita vimechacha mjini Mogadishu

22 Machi 2007

Majeshi ya Somalia yakisaidiwa na yale ya Ethiopia yamefyatuliana risasi na vikosi vya upinzani mjini Mogadishu huku raia wenye wasiwasi wakiutoroka mji huo kwa hofu ya kuzuka mapigano zaidi.

https://p.dw.com/p/CHHi
Askari watiifu kwa serikali ya mpito ya Somalia
Askari watiifu kwa serikali ya mpito ya SomaliaPicha: AP

Raia wanazidi kuutoroka mji wa Mogadishu huku mapigano kati ya wanajeshi wa Somalia wakisaidiwa na wanajeshi wa nchi jirani ya Ethipoia na wapinzani yakiingia katika siku yake ya pili.

Mapigano haya ni makubwa tangu majeshi ya kulinda amani ya umoja wa nchi za Afrika yalipoingia nchini Somalia mapema mwezi huu.

Mamia ya raia wanautoroka mji wa Mogadishu kwa hofu kwa kukodi teksi na mabasi madogomadogo huku baadhi ya jamii masikini wakitimua mbio kwa miguu wakiwa wamebeba mali zao vichwani.

Kaskazini mwa mji wa Mogadishu askari watiifu kwa serikali ya mpito ya Somalia wameshambuliwa karibu na soko la mifugo.

Mapigano makali pia yameripotiwa kusini mwa Mogadishu ambako wapiganani wa kiislamu walijaribu kukata mawasiliano kuelekea kwa wanajeshi wa Ethiopia.

Bi Hadija Mad Osman mama mwenye watoto saba amesema amelazimika kuwaacha mumewe na watoto wake wawili baada ya wao kushindwa kuendelea na safari kutokana na kudhoofika.

Waziri wa mambo ya ndani wa Somalia Mohamed Mohamud Gulled amesema kuwa serikali yake inafanya operesheni itakayo dumu kwa siku saba yenye nia ya kuwafyeka wapinzani kabla ya mkutano wa maridhiano unaotarajiwa kufanyika mwezi April.

Kiongozi wa kundi la wapiganaji wa kiislamu sheikh Dahir Aweys amewataka wasomali kupinga hatua ya kuwepo wanajeshi wa umoja wa Afrika na wale wa kutoka Ethiopia.

Juhudi za umoja wa Afrika za kudhibiti amani na utulivu katika eneo hilo la upembe wa Afrika zinakabiliwa na pingamizi tele nchini Somalia nchi ambayo imekuwa bila ya serikali ya kudumu kwa miaka 16.

Takriban wanajeshi wa kulinda amani 8000 wa AU wanahitajika kupelekwa nchini Somalia lakini hadi sasa mpango huo haujakamilika kwani nchi 53 wanachama wa Umoja wa Afrika hadi sasa zimeahidi kutoa mchango wa wanajeshi 4000 tu.

Tangu mpango wa kulinda amani kuanza Machi 6 ni kikosi cha wanajeshi 1500 tu kutoka Uganda ndicho kimewasili katika mji wa Mogadishu nchini Somalia.

Kapteni Paddy Ankunda msemaji wa kikosi cha Uganda amesema hata hivyo kikosi chake hakihusiki katika mapigano hayo kwani sheria za kikosi cha kulinda amani zinaruhusu tu kujibu mashambulio iwapo kikosi hicho kitashambuliwa.

Serikali ya Somalia imesema kuwa kiongozi wa kundi la kigaidi la Al Qaeda Osama Bin Laden amemtaja kamanda wa kundi la kiislam Aden Hashi Ayro kuwa ni mwakilishi wa kundi hilo mjini Mogadishu.

Balozi wa Marekani nchini Kenya Michael Ranneberger ambae pia anahusika na maswala ya Somalia amesema kuwa Washington inaamini kuwa Ayro anapanga mashambulio dhidi ya serikali ya Somalia na washirika wake hata ingawa ametaja kuwa mashambulio haya ya kila siku hayahusishi kundi la kigadi la Al Qaeda.